Na Silivia Amandius.

Bukoba.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Bukoba Mjini kimeanza rasmi shughuli za kijamii kuelekea maadhimisho ya miaka 49 tangu kuasisiwa kwa chama hicho kwa kutoa msaada wa vifaa mbalimbali kwa vituo viwili vya kulelea watoto yatima vilivyopo katika Manispaa ya Bukoba.

Vituo vilivyonufaika na msaada huo ni Hamugembe na Kashai, ambapo vilipokea mahitaji muhimu yakiwemo mchele, sukari, unga, sabuni pamoja na vifaa vya shule kama madaftari, kalamu na penseli. 

Msaada huo unalenga kuboresha maisha ya kila siku ya watoto wanaolelewa katika vituo hivyo pamoja na kusaidia maendeleo yao kielimu.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Katibu wa CCM Wilaya ya Bukoba Mjini, Shaban Mdohe, alisema chama hicho kimeguswa na hali ya maisha na changamoto zinazowakabili watoto yatima, hususani suala la bima ya afya. 

Ameeleza kuwa Serikali ya Wilaya imechukua jukumu la kufuatilia na kufanyia kazi changamoto hizo ili kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya na ustawi wao unaimarika.

Mdohe aliongeza kuwa utoaji wa msaada huo ni sehemu ya ratiba ya shughuli za kijamii zilizoandaliwa kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya CCM. Shughuli nyingine zilizopangwa ni pamoja na upandaji wa miti, uchangiaji wa damu pamoja na kufanya usafi wa mazingira katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Bukoba.

Kupitia mpango huu, CCM Bukoba Mjini inalenga kuendeleza mshikamano na jamii kwa vitendo, kwa kushiriki moja kwa moja katika kuboresha maisha ya makundi yenye uhitaji maalumu hasa watoto yatima, sambamba na kuhamasisha uwajibikaji wa kijamii kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.