Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga ambaye ni katibu tawala wa wilaya hiyo Gabriel Masinga wakati akizungumza na wanafunzi kuhusu upandaji wa miti.
Mhifadhi wa misitu wilaya ya Sumbawanga Peter Maya wakati akipanda mti.
Na Neema Mtuka, Sumbawanga
Rukwa: Katika kuadhimisha siku ya kumbukizi ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan pamoja na kampeni ya kitaifa ya 27 ya Kijani, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Rukwa wilaya ya Sumbawanga, wamefanya zoezi la kupanda miche 400 ya miti, ikiwemo miti ya matunda, kivuli na mbao, katika eneo la shule ya Msingi Mkuyuni Manispaa ya Sumbawanga Mkoani Rukwa.
Zoezi hilo limelenga kuhamasisha uhifadhi wa mazingira, kurejesha uoto wa asili na kuimarisha juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuunga mkono dira ya Taifa ya uendelevu wa mazingira.
Mhifadhi wa misitu wilaya ya Sumbawanga, Adolph Peter Maya, ambaye alikuwa miongoni mwa waliopanda miti katika shule ya msingi mkuyuni, alisema kuwa upandaji miti ni sehemu ya mkakati endelevu wa kulinda rasilimali za misitu na kuhakikisha mazingira salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.
“Ushirikiano kati ya taasisi za serikali, mashirika binafsi na jamii ni muhimu kufanikisha agenda ya uhifadhi wa mazingira. Kupanda miti ni hatua ndogo yenye manufaa makubwa kwa vizazi vijavyo,” alisema Maya.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga ambae ni katibu tawala wa wilaya ya Sumbawanga Gabriel Masinga alisema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika shughuli za kijamii na kimazingira, huku akibainisha kuwa upandaji miti ni uwekezaji wa muda mrefu unaochangia afya ya mazingira na maendeleo endelevu ya jamii.
Zoezi la upandaji miti Mashuleni ni miongoni mwa shughuli mbalimbali zinazofanywa katika maadhimisho ya 27 ya Kijani, yaliyolenga kuongeza uelewa wa jamii juu ya umuhimu wa kulinda misitu, kuhifadhi rasilimali asilia, na kuchukua hatua za vitendo katika utunzaji wa mazingira.
“Kila mti unaopandwa ni mchango wa moja kwa moja katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongeza uoto wa asili na kuhakikisha vizazi vijavyo vinaishi katika mazingira bora,” alifafanua Masinga.
Hii inatokana na juhudi za TFS za kuhakikisha kwamba miche, elimu na ushauri wa kitaalamu vinapatikana kwa jamii, jambo linalosaidia kuhakikisha kila zoezi la upandaji miti linafanikiwa kwa uendelevu.
