NA DENIS MLOWE, IRINGA
KATIKA kikao kizito kilichowakutanisha viongozi wa michezo wa mkoa , Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James ametoa wito wa dharura kwa wadau kujipanga upya na kuchukua hatua madhubuti katika kuinua michezo, hususan soka, ambacho kimeonekana kuwa mchezo unaopendwa na kuungwa mkono na wananchi wengi wa mkoa huo.
Akizungumza mbele ya viongozi wa wilaya, makatibu tawala, maafisa michezo, maafisa elimu, walimu wa shule za msingi na sekondari, pamoja na viongozi wa vyama vya michezo, Mkuu wa Mkoa alisema imefika wakati suala la michezo lisichukuliwe kwa uzito mdogo kwani ndilo linalobeba furaha, burudani na heshima ya mkoa.
“Nimekaa kimya kwa muda mrefu nikiangalia ni kwa jinsi gani mmejipanga. Lakini kadri siku zinavyoenda, sioni mipango madhubuti. Sasa inabidi nijitokeze mwenyewe. Waswahili wanasema: ‘Usipo uanika utaula mbichi’, na ndiyo maana kabla hatujala mbichi, tufanye kazi ya kuuanika,” alisema.
Mkuu wa mkoa alisisitiza kuwa Iringa imebarikiwa kuwa miongoni mwa mikoa yenye mapenzi makubwa kwa michezo, na kwamba kutokuwepo kwa mikakati endelevu kwa muda mrefu kunawanyima wananchi haki yao ya kujiburudisha na kujivunia michezo yao.
Aidha, alieleza kuwa mkoa una historia ndefu ya michezo, na hivyo uongozi na wadau wanapaswa kuhakikisha urithi huo unaendelezwa, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha mazingira ya kuibua na kukuza vipaji.
Katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa aliainisha maeneo matatu muhimu ambayo mkoa unaweza kuamua kuyawekea nguvu ili kufikia maendeleo ya haraka:
Alisema kuwa eneo la kwanza ni Kuzalisha wachezaji bora Iringa inatambulika kwa kutoa vijana wenye uwezo mkubwa katika soka, hivyo mkoa unaweza kujiweka kwenye ramani ya kitaifa kama kitovu cha vipaji.
Alibainisha eneo la pili kuwa ni Ujenzi wa miundombinu ya michezo mkoa unaweza kuwa kambi ya timu za ndani na nje ya nchi iwapo utawekeza ipasavyo katika viwanja na vifaa vya kisasa vya michezo.
Alisema eneo la tatu ni Kuimarisha timu za ushindani kuwa na timu zenye uwezo wa kushindana kitaifa na kimataifa kutatoa hamasa kwa vijana na kuongeza hadhi ya mkoa.
“Nimekuja kutoka Mwanza hadi hapa Iringa, kazi yangu ni kuhakikisha vijana wenu wanapata nafasi ya kufika mbali. Mna historia ya kuzalisha wachezaji bora na hilo ni jambo la kujivunia,” aliongeza.
Alimaliza kwa kuwataka viongozi wote wa michezo kuacha kukaa pembeni na badala yake washiriki kikamilifu katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia ajenda za michezo ili kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa vitendo.
Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Iringa, Adinan Chorobi, amesema kuwa Mkoa wa Iringa umeendelea kuwa na historia ndefu na ushiriki mpana katika ngazi zote za ligi za Tanzania.
Amesema kuwa, kwa kipindi kirefu,Iringa imekuwa na timu zinazoshiriki ligi mbalimbali ikiwemo Ligi Daraja la Pili (sasa First League), Ligi Daraja la Kwanza (sasa Championship), pamoja na Ligi Kuu (NBC Premier League). Amesisitiza pia kuwa upande wa wanawake, Iringa imekuwa ikiwakilishwa na timu za ushindani kama Iringa United Queens na Ceaseac Queens, ambapo kwa sasa ndiyo inayobaki kuwa mwakilishi wa Mkoa katika Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara.
Chorobi amebainisha kuwa hali halisi ya soka mkoani Iringa ina changamoto zake, licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na chama kusimamia na kuratibu michezo kuanzia ngazi ya wilaya hadi mkoa.
“Majukumu yetu ni kusimamia michezo yote inayochezwa ndani ya mkoa, kuhakikisha ligi zinaendeshwa kwa mujibu wa kanuni na kupata mabingwa halali,” alisema.
Akitoa mfano wa mafanikio ya karibuni, Chorobi amesema chama kimemaliza ligi ya mkoa na kumpata bingwa mpya, Hits .
Chorobi ametaja changamoto ya ukosefu wa fedha kama kikwazo kikubwa kinachozifanya timu nyingi za Iringa kushindwa kufanya vizuri.
Amesema timu nyingi zinakabiliwa na ukata, jambo linalosababisha ugumu katika uendeshaji, usajili, maandalizi na kushindwa kutekeleza mikakati ya maendeleo.
Aidha, Katibu huyo ameeleza kuwa moja ya sababu kubwa zinazokwamisha maendeleo ya vilabu mkoani ni aina ya viongozi wanaoongoza timu. “Tatizo kubwa la vilabu vyetu ni viongozi waliopewa dhamana ya kuvisimamia. Uongozi usio makini na usio wa uwaminifu umewakatisha tamaa wadau wengi ambao walikuwa tayari kusaidia. Hali hii imepelekea baadhi ya timu kufa vifo vya kawaida,” alisema Chorobi.
Amesema pia kuwa chama kimekuwa kikifanya jitihada za ushauri na miongozo ya uendeshaji wa vilabu, ikiwemo kufanya vikao na viongozi wa timu, lakini mara nyingi maazimio haya hayatekelezwi wanapotoka kwenye vikao. “Chama hakiwezi kuchukua majukumu ya kuendesha timu. Sisi ni wasimamizi na walezi; jukumu la uendeshaji linabaki kwa viongozi wa timu na wanachama wao,” alisisitiza.
Katibu Chorobi amehitimisha kwa kusisitiza kuwa udhaifu wa kiuongozi ndani ya vilabu ndiyo changamoto kuu inayorudisha nyuma maendeleo ya mpira wa miguu mkoani Iringa.
Akatoa wito kwa viongozi wa timu, wanachama na wadau kuwekeza katika uongozi bora, uwajibikaji na mipango endelevu ili kufikia mafanikio ya kudumu katika mchezo huo.
Mkuu wa mkoa Kheri alisema kuwa ataitisha kikao kikubwa cha wadau wa soka ili kupata njia sahihi ya kukuza soka mkoani hapa.

