NA DENIS MLOWE, IRINGA

 

KANISA la New Life in Christ – (Maisha Mapya Ndani ya Kristo) kwa kushirikiana na Diwani wa Viti Maalum kanda ya Kihesa, Sarah Ponela, wametoa madawati 100 kwa shule mbalimbali zilizopo katika Wilaya ya Iringa zenye uhitaji mkubwa, ikiwa ni mchango wa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha sekta ya elimu.

Madawati hayo yenye thamani ya shilingi milioni 10 yamekabidhiiwa kwa Mkuu wa wilaya ya Iringa ambaye atakayakabidhi katika shule zenye upungufu mkubwa wa madawati ambapo yatasaidia watoto zaidi ya 300.

 

Akisoma risala mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, Katibu wa Kanisa hilo, Akson Lufyagila, alisema kanisa hilo lenye zaidi ya waumini 2,000 mkoani Iringa limekuwa mstari wa mbele kusaidia makundi maalum na jamii kwa ujumla. Alinukuu Mithali 19:17, “Amhudumiaye maskini amemkopesha Bwana,” akibainisha kuwa madawati hayo yatanufaisha zaidi ya wanafunzi 300.

 

Lufyagila alitaja pia maombi ya kanisa kwa serikali, likiwemo ombi la kupatiwa eneo la kujenga kituo cha kulelea wazee, ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji, pamoja na kuboreshewa barabara inayoelekea kanisani kwao lililopo Kata ya Gangilonga, eneo la Wilolesi.

 

Kwa upande wake, Diwani Sarah Ponela alisema mchango huo ni sehemu ya kusaidia jitihada za serikali, hususan mafanikio ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan.

 

Aidha, alimtambulisha Charles Kihavangu, fundi mwenye ulemavu aliyetengeneza madawati hayo, akisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika fursa za kazi na kujiongezea kipato.

 

Akizungumza kama mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, alilishukuru kanisa hilo na kuwataka wadau wengine wa maendeleo kuiga mfano huo.

 

Akirejea Matendo ya Mitume 4:32–35, alisema huo ndio “mfano halisi wa kanisa linalogusa wenye mahitaji.”

 

Kuhusu maombi yaliyowasilishwa na kanisa, Sitta alisema yanahitaji mazungumzo zaidi, huku akimuagiza Mhandisi wa TARURA kukagua barabara inayoelekea kanisani kwa lengo la kuona namna ya kuifanyia maboresho.

Aidha Sitta alisema kuwa kama serikali itaendelea kushirikiana na makanisa na misikiti pale ambapo wanahitaji kufanya jshughuli za kijamii na kitendo cha mlemavu kutengeneza madawati hayo amesema kuwa ataangalia kwa jicho la tatu katika kumpatia mkopo inayotolewa na Halmashauri.