Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma, wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Khalid Khalif jana,wakati wa kikao cha robo ya pili cha Baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri hiyo(Picha na Muhidin Amri)
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma Khalid Khalif,akitoa taarifa mbalimbali kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza la madiwani kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo,kulia kwake Mwenyekiti wa Halmashauri Stewart Nombo(Picha na Muhidin Amri).
………….
Na Mwandishi Wetu Nyasa
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma,wamesisitizwa kuwa wabunifu kwa kuibua,kutafuta vyanzo vipya vya mapato na kudhibiti utoroshaji wa mapato hasa yanayokusanywa katika maeneo yao.
Wito huo umetolewa jana na Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Peres Magiri,katika hotuba yake iliyosomwa na Afisa Tawala wa Wilaya hio Benedicto Nsindagi kwenye kikao cha robo ya pili cha Baraza la madiwani kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri Wilayani humo.
Aliongeza kuwa,ukusanyaji wa mapato lazima uendane na nidhamu ya matumizi sahihi ya fedha hivyo madiwani wahakikishe wanasimamia ipasavyo mapato yote yanayopatikana kupitia vyanzo vilivyopo.
“Suala la mapato ni muhimu kwani ndiyo uti wa mgongo wa Halmashauri,nawaomba sana waheshimiwa madiwani wapya na wale wa zamani mkasimamie mapato na kuibua vyanzo vipya ambavyo vitawezesha Halmashauri yenu kujitegemea badala ya kusubiri kupokea fedha kutoka Serikali kuu na wadau wengine”alisema Magiri.
Magiri,amewataka madiwani kuwa na utaratibu wa kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa katika maeneo yao ili kujiridhisha kama inalingana na gharama halisi ya fedha zinazotolewa badala ya kuwa watazamaji.
“Madiwani kupitia kamati zenu hakikisheni mnafuatilia na kufanya ukaguzi wa miradi inayotekelezwa kwenye kata zenu ili mjiridhishe kama kweli inalingana na fedha zinazotolewa na Serikali hususani kwenye ubora badala ya kuwa watazamaji”alisema Magiri.
Amewaasa madiwani,kwenda kushirikiana na kuwalinda watumishi na kuepuka kuwa chanzo cha migogoro kati ya watumishi,Serikali na wananchi ambayo inapelekea kushusha hali ya utendaji kazi kwa watumishi.
Pia,amewataka watumishi na wakuu wa idara kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kujenga imani kwa wananchi na kuepuka tabia zisizoendana na maadili ya utumishi wa umma kama vile kuzalisha migogoro na chuki baina ya Serikali na wananchi.
Akizungumzia kuhusu sekta ya elimu Magiri,ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha nyingi ambazo zimewezesha kuboresha mazingira na miundombinu ya elimu na kuagiza watoto wote wenye sifa ya kuanza elimu ya awali,msingi na kidato cha kwanza hakuna anayebaki nyumbani.
Alisema,Serikali imejitahidi kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na miundombinu mingine kwa hiyo kama wazazi hawatapeleka watoto wao shule fedha hizo hazitafanya kazi iliyokusudiwa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Stewart Nombo,amehaidi Halmashauri kwenda kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Serikali ikiwemo usimamizi na utekelezaji wa miradi na mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani.
Nombo alisema,hadi kufikia tarehe 30 Desemba 2025 Halmashauri hiyo imekusanya asilimia 65 kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato yake na mategemeo kuwa ifikapo tarehe 30 Juni, watafikisha asilimia zaidi ya 100.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Nyasa Khalid Khalif,amewapongeza wananchi na viongozi wa Tarafa ya Mpepo kwa jitihada kubwa wanazofanya katika usimamizi na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo hususani miradi ya elimu.
Khalif,amewataka wananchi kutambua kwamba miradi inayotekelezwa ni yao,hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake na kuwa walinzi wa miradi hiyo badala ya kuichia Serikali.
Diwani wa kata ya Lituhi Benjamin Mahena,ameipongeza Ofisi ya Mkurugenzi kwa matumizi mazuri ya fedha na kuzitaka idara nyingine kuwa na matumizi sahihi ya fedha na kushauri fedha zilizobaki kwa mwaka wa fedha 2024/2025 zipelekwe kwenye vikundi vya ujasiriamali ili kuviongezea nguvu.




