Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Mhe. Husna Sekiboko (Mb), akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA wilayani Chemba, mkoani Dodoma, Januari 24, 2026.
Na. Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Serikali imehimizwa kuimarisha sera na mifumo ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi ili kuhakikisha ujuzi wanaoupata unatumika moja kwa moja katika uzalishaji na kutatua changamoto za kijamii. Hatua hiyo imeelezwa kuwa msingi muhimu wa kupunguza ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
Wito huo umetolewa Januari 24, 2026, na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ziara yake katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) cha Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Husna Sekiboko, amesema kuwa licha ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya elimu ya ufundi stadi, bado kuna changamoto ya wahitimu kushindwa kuendeleza ujuzi wao kutokana na ukosefu wa mitaji na zana za kazi.
Amesema uwezeshaji wa kifedha kwa wahitimu utasaidia kubadili elimu ya ufundi stadi kuwa chombo cha moja kwa moja cha kutatua changamoto za kijamii na kukuza uchumi wa wananchi, badala ya kuishia katika umiliki wa vyeti.
Aidha amebainisha kuwa ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi unapaswa kuendelea kupewa kipaumbele sambamba na uwekezaji wa Serikali, akisisitiza kuwa majengo, vifaa vya kufundishia na mifumo ya TEHAMA lazima yaendane na mitaala ya kisasa pamoja na walimu wenye weledi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, amebainisha kuwa mageuzi yaliyofanyika katika vyuo vya VETA yameongeza upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi hadi ngazi ya wilaya, hali iliyochangia kuongeza idadi ya vijana wanaopata mafunzo ya ufundi na kuifanya sekta hiyo kuwa mhimili wa maendeleo ya rasilimali watu.
“Bila kuzingatia ubora wa mafunzo, uwekezaji wa fedha pekee hauwezi kuleta tija iliyokusudiwa. VETA inapaswa kuhakikisha kila rasilimali inayowekezwa inaleta wahitimu wenye ujuzi unaotumika katika jamii na kuchangia uchumi wa taifa,” amesema.
Aidha, Mhe. Husna Sekiboko ameipongeza Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kwa kazi kubwa na nzuri inayofanya katika kukuza elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Elimu , Sayansi na Teknolojia , Mhe.Wanu Hafidh, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya mafunzo, mitaala na mifumo ya ufundi stadi ili kuhakikisha vijana wanabadili ujuzi wao kuwa fursa za kiuchmi.
Baadhi ya Wajumbe Kamati hiyo, wametoa ushauri na maoni Yao,Mhe.Bakar Shingo, Mbunge wa Jimbo la Ukonga Jijini Dar es salaam,amesema kuwa kuna umuhimu wa kuboresha miundombinu ya maji katika chuo cha VETA Chemba pamoja na ujenzi wa uzio ili kuimarisha usalama wa wanafunzi na mali za chuo.
Aidha amebainisha kuwa kuanzishwa kwa kozi zinazozingatia mazingira ya Wilaya ya Chemba kutawawezesha vijana kupata ujuzi unaowawezesha kujiajiri na kuchangia moja kwa moja maendeleo ya eneo hilo.
Kwa upande mwingine, mjumbe wa Kamati hiyo, Mhe.Asha Baraka, amesema kuwa kuna haja ya VETA kubuni mafunzo yanayolenga mahitaji halisi ya jamii, ikiwemo upatikanaji wa maji safi, nishati ya umeme, makazi bora na huduma za msingi.
Aidha amebainisha kuwa mafunzo ya ufundi wa kutengeneza viatu yanaweza kuwa fursa kubwa ya ajira kwa vijana endapo yataandaliwa kwa kuzingatia mazingira ya ndani, uwezo wa kiuchumi wa wananchi na ubora wa bidhaa zinazozalishwa.
Amesema ufundi wa viatu unaweza kuunganishwa na ubunifu wa kisasa pamoja na matumizi ya malighafi za ndani, hali itakayopunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuongeza kipato cha vijana hasa walioko vijijini.
Akizungumza kwa niaba ya VETA, Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, CPA Anthon Kasore, amesema mamlaka hiyo inaendelea kuimarisha upatikanaji wa elimu ya ufundi stadi kwa usawa, kuboresha ubora wa mafunzo na kuendeleza ubunifu ili kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi unaoendana na vipaumbele vya taifa.
Amesema kati ya mwaka 2021 hadi 2026, jumla ya wanafunzi 430,416 wamedahiliwa katika vyuo vya VETA nchini, wakiwemo wanafunzi wenye mahitaji maalum na wanaotoka katika mazingira magumu.
Aidha amebainisha kuwa kupitia Mpango wa Ukuzaji Ujasiriamali katika Sekta Isiyo Rasmi (INTEP), wajasiriamali 6,515 wamepatiwa mafunzo maalum ya kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Aidha, CPA Kasore amesema vyuo 59 pamoja na ofisi za kanda za VETA zimeunganishwa na mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, huku vyuo 26 vikiwekewa nishati safi ya kupikia kama sehemu ya mkakati wa kulinda mazingira.
Akizungumzia Chuo cha VETA Chemba, amesema chuo hicho ni miongoni mwa vyuo 25 vya wilaya vilivyojengwa na Serikali kati ya mwaka 2020 na 2023 kwa lengo la kusogeza elimu ya ufundi stadi karibu na wananchi.
Amesema kwa sasa chuo hicho kinatoa mafunzo katika fani sita na kimedahili wanafunzi 115, wakiwemo wanaume 69 na wanawake 46, huku kikiwa na jumla ya wafanyakazi 19.
Aidha, amebainisha kuwa VETA inaendelea kushirikiana na PPRA ili kuhakikisha vikundi vya wahitimu vinapata usajili rasmi, vitendea kazi na fursa za ujasiriamali.
Kwa Upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Hussein Omar, amesema Wizara inaendelea kutathmini njia bora za kuwawezesha wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi kupata mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Ameir Hafidh (Mb), akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo katika Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA wilayani Chemba, mkoani Dodoma, Januari 24, 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthon Kasore, akifafanua Jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ziara yao katika Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA wilayani Chemba, mkoani Dodoma, Januari 24, 2026.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthon Kasore, akifafanua Jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo wakati wa ziara yao katika Chuo cha Ufundi Stadi cha VETA wilayani Chemba, mkoani Dodoma, Januari 24, 2026.





