Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog,
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitaruhusu historia, ukweli na mafanikio ya taifa kuchafuliwa au kupotoshwa kwa maslahi ya watu binafsi.
Haya yamesemwa na Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Ndg. Kenan Kihongosi, wakati akizungumza na waandishi wa habari Januari 17, 2026 jijini Dodoma.
Amesema kuwa CCM itaendelea kusimamia misingi yake kwa kuhakikisha ukweli wa historia ya taifa na mafanikio yaliyopatikana yanabaki kulindwa, huku chama kikiimarisha uhusiano wake na wananchi kupitia kusikiliza na kutatua changamoto zao.
Aidha, Kihongosi , amesema kuwa chama kinatarajiwa kuanza ziara ya kimkakati nchi nzima itakayozinduliwa rasmi Januari 19, 2026 wilayani Manyoni mkoani Singida. Amesema kuwa ziara hiyo itahusisha kutembelea wilaya zote za Mkoa wa Singida pamoja na kufanya mikutano ya hadhara.
Amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini, kusikiliza kero zao na kuzitatua, kuisimamia Serikali, kuimarisha uimara wa chama, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Aidha amebainisha kuwa kupitia ziara hiyo, chama kitafuatilia utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizozitoa wakati wa kampeni, ikiwemo ahadi zilizopangwa kutekelezwa ndani ya siku 100, ili kubaini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake au matarajio ya lini zitatekelezwa.
Pia, Amebainisha kuwa ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa CCM wa kuendelea kuimarisha uwajibikaji wa Serikali na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati na kwa mujibu wa mipango iliyopo.

