Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala wakiwa katika utekelezaji wa majukumu ya kuokoa na kuzima moto katika ajali ya moto iliyotokea leo Januari 16, 2026 katika jengo la gorofa tisa linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), lililopo Posta, Mitaa ya Azikiwe na Samora, jijini Dar es Salaam.




………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Jengo la gorofa tisa linalomilikiwa na Shirika la Hifadhi ya Taifa ya Jamii (NSSF), lililopo Posta, Mitaa ya Azikiwe na Samora, jijini Dar es Salaam, limenusurika kuungua baada ya moto mkubwa kuzuka katika jengo hilo.
Akizungumza na mwandishi wetu leo jijini Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala, Frank Mwalongo, amesema kuwa majira ya saa sita na robo mchana walipokea wito wa dharura kuhusu ajali ya moto katika jengo la NSSF, na walifanikiwa kufika eneo la tukio kwa wakati na kudhibiti moto huo.
Mwalongo amesema kuwa katika tukio hilo, Jeshi la Zimamoto lilifanikiwa kudhibiti moto huo kabla haujasababisha uharibifu mkubwa, hivyo kuepusha jengo hilo kuungua.
Aidha, amesema kuwa watu wawili walijeruhiwa katika tukio hilo na wameokolewa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Ameongeza kuwa chanzo cha moto huo bado hakijafahamika, huku akieleza kuwa uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo.
Kwa upande wao mashuhuda wa tukio hilo, Rehema John na Jackson Emmanuel, wamesema kuwa moto ulianza kuwaka katika sehemu ya chini ya jengo na kusambaa kuelekea juu, hali iliyosababisha taharuki miongoni mwa wafanyakazi na wananchi waliokuwepo karibu na jengo hilo.
Mashuhuda hao wamekipongeza Jeshi la Zimamoto na vyombo vingine vya usalama kwa kufika kwa wakati na kufanikiwa kuwaokoa watu waliokuwamo ndani ya jengo hilo, hususan waliokuwepo katika gorofa za juu.




