Na John Bukuku – Dar es Salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema Serikali itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Asha-Rose Migiro, wakati wa ziara yake ya wiki nzima mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee Januari 23, 2026, Mgogoro amesema kuwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, watumishi na watendaji wote wa Serikali wamejipanga kuyatekeleza na kuyaishi maelekezo yote yaliyotolewa, ikiwemo kusimamia vyema Ilani ya CCM kwa kushirikiana na uongozi wa chama hicho.
Mhe. Edward Mpogolo amesema Wilaya ya Ilala imepata mafanikio makubwa ya maendeleo yanayotokana na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 317 zimeletwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Amesema katika sekta ya afya, zaidi ya shilingi bilioni 107 zimeelekezwa, zikijumuisha ujenzi wa vituo vya afya, kikiwemo kituo kimoja kilichofikia hatua za mwisho za ujenzi na kinatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi huo. Aidha, amebainisha kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kujenga vituo vipya vitano vya afya vya kisasa katika maeneo ya Pugu Kinyamwezi, Pugu Stesheni, Vingunguti, Mongola Ndege na Kisukuru, ambapo michoro imeshakamilika na kuthibitishwa na TAMISEMI.
Katika sekta ya elimu, Mpogolo amesema zaidi ya shilingi bilioni 36 zimeelekezwa kwenye elimu ya sekondari na zaidi ya shilingi bilioni 1 kwenye elimu ya msingi. Amesema kuwa zaidi ya madarasa 600 ya shule za msingi na madarasa zaidi ya 500 ya shule za sekondari yamejengwa au yako katika hatua za ujenzi. Aidha, amebainisha kuwa shule mpya za sekondari zimejengwa, ikiwemo Shule ya Sekondari Kitunda Relini yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.1, ikiwa na madarasa 16, ofisi pamoja na maabara zote muhimu.
Aidha, amebainisha kuwa shule nane za sekondari za ghorofa zinaendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ilala, ikiwemo shule ya sekondari inayojengwa karibu na Ofisi za CCM Lumumba.
Katika sekta ya miundombinu, Mpogolo amesema zaidi ya shilingi bilioni 134 zimetolewa kupitia Mradi wa DMDP kwa ajili ya ujenzi wa barabara, pamoja na zaidi ya shilingi bilioni 36 kwa ajili ya ujenzi wa tenki la maji la Bangulo.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mshikamano wa viongozi wa CCM wilayani humo wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Said Side, viongozi wa Mkoa, Madiwani, Mbunge pamoja na Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Aidha, amebainisha kuwa Wilaya ya Ilala ilimpatia Rais zaidi ya kura milioni 1.2, jambo linaloonesha imani kubwa ya wananchi kwa uongozi wake.
Mpogolo amesema mafanikio hayo yote yanapatikana chini ya uongozi na usimamizi wa Chama Cha Mapinduzi, akiwataja Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Kamati ya Siasa ya Mkoa, MNEC wa Mkoa pamoja na Katibu wa Itikadi na Uenezi Mkoa, Kenani Kihongosi, kuwa ni nguzo muhimu ya maendeleo hayo.
Pia, amebainisha kuwa Wilaya ya Ilala itaendelea kuimarisha mshikamano na kuwatumikia wananchi kwa unyenyekevu na uungwana, akisisitiza kuwa wananchi ndio waliokichagua Chama Cha Mapinduzi pamoja na viongozi wake.

