Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Asha-Rose Migiro, amesema uimara na uhai wa chama hicho haujengwi kupitia majukwaa ya mikutano bali huanzia kwenye ngazi ya mashina na matawi, ambako ndiko kunakoweka misingi halisi ya chama.
Dk. Migiro ametoa kauli hiyo leo Januari 9, 2026, alipokuwa akizungumza na viongozi wa mashina na matawi wa Wilaya za Kinondoni na Ubungo, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake kwa viongozi wa ngazi za chini za chama jijini Dar es Salaam.
Amesema majukwaa ya mikutano hutumika zaidi kwa ajili ya kutoa hamasa, lakini ujenzi wa chama kwa maana ya mshikamano, nidhamu na uhai wake halisi huanzia kwenye mashina ambako chama hukutana moja kwa moja na wananchi.
Akisisitiza zaidi, Dk. Migiro amesema nguvu ya CCM ipo kwenye mashina kwa kuwa ndiko kunakojengwa misingi ya chama, kuimarishwa itikadi na kulelewa wanachama wanaokitumikia chama kwa uaminifu.
Aidha, ametoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi zote kuhakikisha wanashiriki kikamilifu vikao vya mashina, akibainisha kuwa vikao hivyo vina mchango mkubwa katika kuimarisha uhai wa chama na kuimarisha uhusiano kati ya CCM na wananchi.
“Mashina ndiyo moyo wa CCM kwa kuwa ndiyo yanayokutanisha chama na wananchi moja kwa moja kupitia vikao na shughuli mbalimbali za kijamii na kisiasa,” amesisitiza Dk. Migiro, ambaye anaendelea na ziara yake Dar es Salaam chini ya kauli mbiu ‘Shina lako linakuita’.
Ameongeza kuwa vikao vya mashina vina mchango mkubwa katika kuyakomaza mashina, ambayo baadaye hukua na kuwa matawi imara na hatimaye kujenga chama chenye misingi thabiti na endelevu.




