Waziri Mkuu wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewaonya Watanzania dhidi ya kuingia kwenye kile alichokitaja kuwa ni mtego wa migogoro ya kidini, akisisitiza kuwa migogoro inayogusa imani za watu haina mshindi na inaweza kulivuruga taifa zima endapo haitakwepwa mapema.

Akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam leo, Desemba 29, 2025, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko na kituo cha mabasi Bunju, Wilaya ya Kinondoni, Dkt. Nchemba amesema mataifa mengi yanayoendelea yamekuwa yakitegewa mitego katika vipindi vya uchaguzi kwa kuchochewa ukabila na udini.

Ameeleza kuwa Tanzania imefanikiwa kuvuka mtego wa ukabila, lakini sasa inakabiliwa na hatari ya mtego wa udini, hali inayohitaji tahadhari ya hali ya juu kutoka kwa viongozi na wananchi kwa ujumla.

Dkt. Nchemba amesema Tanzania imejengwa juu ya misingi ya kuvumiliana kidini, ambapo serikali haina dini na kila mwananchi ana uhuru wa kuabudu dini anayoamini bila vikwazo, hali iliyowezesha hata familia zenye waumini wa dini tofauti kuishi kwa amani.

“Ukigusa imani ya mtu, hapo hakuna mshindi. Ukishaingia kwenye mtego huu hauna kutoka,” amesema Dkt. Nchemba, akionya kuwa migogoro ya kidini ikianza huwakumba wote bila kujali nani alichochea au nani alikaa kimya.

Waziri Mkuu amewahimiza viongozi wa dini, viongozi wa siasa pamoja na wananchi wa kawaida kutumia njia sahihi za mazungumzo na ushauri pale wanapokuwa na hoja au malalamiko, akisisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameweka wazi milango ya mazungumzo na yuko tayari kupokea mawazo, ushauri na hoja kutoka kwa wadau mbalimbali.

Aidha, ameonya dhidi ya tabia ya kushambuliana hadharani katika masuala ya imani, akieleza kuwa kiongozi wa dini anaposhambuliwa, waumini wake humtazama kama baba au kiongozi wa kiroho, jambo linaloweza kuchochea hasira na migawanyiko mikubwa katika jamii.