NA DENIS MLOWE, IRINGA
WANAFUNZI waliosoma Shule ya Msingi Ipogoro na kuhitimu mwaka 2001 wametoa msaada wa madawati 32 kwa shule hiyo kama sehemu ya kurudisha fadhila na kuunga mkono jitihada za kuboresha elimu katika eneo hilo.
Msaada huo umetolewa baada ya wahitimu hao kuguswa na changamoto kubwa ya upungufu wa madawati, hali iliyokuwa ikichangia msongamano darasani na kuathiri mazingira bora ya kujifunzia.
Kiongozi wa kundi la wahitimu hao, Denis Milele ambaye pia ni Mkurugenzi wa Maduka ya vifaa vya michezo ya Milele, alieleza kuwa kitendo hicho ni ishara ya upendo wao kwa shule iliyowajenga na kuwafungulia milango ya mafanikio katika maisha yao ya sasa.
Milele ambaye aliambatana na wanafunzi wenzake waliojichanga katika kufanikisha kupatikana madawati hayo , alisema kuwa wanatambua mchango mkubwa wa walimu waliowafundisha, hivyo msaada huo ni mwanzo tu wa safari yao ya kuendelea kuiunga mkono shule hiyo kwa kadri watakavyoweza.
Aliongeza kuwa wahitimu hao wa 2001 wamejipanga kusuka mipango mingine ya kufanya maendeleo ya mara kwa mara ili kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa rafiki kwa kizazi cha sasa na kuweza kuwakuza katika msingi wa kutoa .
Akipokea msaada huo, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ipogoro, Kenan Chalamila, aliwapongeza wahitimu hao kwa moyo wa kujitoa na kwa kumbukumbu yao njema kwa shule iliyowalea.
Chalamila alisema kuwa madawati hayo yatapunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la wanafunzi kukaa watatu hadi wannei kwa dawati moja na hivyo kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Alisema kuwa wanaupungufu wa madwati 175 ambapo wanafunzi wamekuwa wakikaa watatu hadi wanne ambapo alisema shule hiyo ina wanafunzi zaidi ya 1000 na walimu 32.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ruaha ambapo shule ya msingi Ipogoro ipo, Musa Mbungu, aliwashukuru wahitimu hao kwa kuonyesha mfano bora wa uzalendo na kuwataka wananchi wengine kuiga moyo huo wa kusaidia taasisi za elimu.
Mbungu aliahidi kuendelea kushirikiana na uongozi wa shule na wadau mbalimbali ili kuhakikisha miundombinu ya shule ya Ipogoro inaendelea kuimarika kwa manufaa ya wanafunzi na jamii nzima.
Alisema kuwa serikali imetoa milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa shue hiyo mwemye majengo 10 ambapo ujenzi unaendelea kwani shule hiyo ni moja ya shule konngwe mkoani hapa.





