Wananchi wameeleza kuwa shule hiyo itasaidia kupunguza changamoto za kijamii zilizokuwa zikiwakumba watoto, hususan wasichana, waliokuwa wakikabiliwa na hatari mbalimbali kutokana na umbali wa shule.
Mwananchi Vumilia Chegamila amesema ukaribu wa shule umeleta faraja kwa wazazi na wanafunzi, kwani utarahisisha usimamizi wa watoto na kupunguza gharama na changamoto zilizokuwepo awali.
“Ukaribu wa shule utatusaidia sisi wazazi kutimiza mahitaji ya watoto wetu kwa urahisi zaidi, tofauti na hapo awali ambapo umbali ulikuwa changamoto kubwa,” alisema.
Aidha, wananchi wamepongeza uwepo wa miundombinu bora ikiwemo madarasa ya kisasa na mazingira rafiki ya kujifunzia yanayotarajiwa kuongeza bidii na ufaulu kwa wanafunzi wa Kata ya Isakalilo.
Ujenzi wa shule hiyo unaendelea kuchukuliwa kama hatua muhimu ya maendeleo ya elimu katika Manispaa ya Iringa, hasa kwa wakazi wa Mtaa wa Kitasengwa na maeneo ya jirani.
Afisa Mtendaji Kata ya Isakalilo Bryson Muhugumu amesema shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi muhula wa kwanza wa mwaka 2025 pindi shule zitakapofunguliwa rasmi, huku akiwahimiza wazazi na walezi kuanza maandalizi mapema kwa ajili ya kuwasajili watoto wao katika shule hiyo na kumpongeza mwekezaji Daniel Kalinga kuwekeza shule kwenye kata hiyo.
Alisema kuwa uwepo wa shule hiyo utasaidia kupanuka kwa mji huo na kuwataka wananchi kujitokeza kununua viwanja katika eneo la Kitasengwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shule, Mugabe Kihongosi, amesema uwekezaji huo unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu, akibainisha kuwa shule hiyo imejengwa kwa viwango vinavyokidhi mahitaji ya elimu ya sasa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Shule ya Awali na msingi ya Kaldan , Daniel Kalinga
amesema kuwa uamuzi wa kujenga shule hiyo kufuatia kuongezeka kwa mahitaji ya elimu ya watoto wadogo, hususan elimu ya Kiingereza, kunakotokana na ukuaji wa kasi wa Manispaa ya Iringa na eneo la Kitasengwa.
Akizungumza katika hafla maalum ya uzinduzi wa shule hiyo iliyowakutanisha wananchi wa kata hiyo amesema wazo la kuanzisha shule hiyo lilianza mwaka 2014 baada ya kukutana na Mzee John Kilekauhate Galate, ingawa utekelezaji wake umefanyika kwa sasa baada ya maandalizi ya muda mrefu.
Amesema Shule ya Awali na Msingi KALDAN itafunguliwa rasmi tarehe 13 Januari, 2025, na kwa sasa zoezi la ugawaji wa fomu za kujiunga linaendelea. Mkurugenzi huyo aliishukuru jamii kwa mwitikio mkubwa na kuahidi kuwa shule hiyo itatoa elimu bora na malezi yanayokidhi viwango vinavyotakiwa.
“Tumefanikiwa kujenga miundombinu ya shule, lakini tunatambua kuwa majengo bila elimu bora ni kazi bure. Hivyo, uongozi wa shule, walimu, wazazi na wanafunzi tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha ndoto ya shule hii inafikiwa,” alisema.
Kupitia hafla hiyo, uongozi wa KALDAN umeomba ushirikiano na imani kutoka kwa wazazi na jamii kwa ujumla kwa kuwaleta watoto wao ili wapate malezi na elimu ambayo ni msingi wa maisha ya mwanadamu.
Mkurugenzi huyo alitoa ahadi mbele ya hadhara kuwa atatumia uwezo na maarifa yake yote, kwa msaada wa Mungu, kuhakikisha shule hiyo inakuwa miongoni mwa shule bora katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa shule ya Awali na Msingi Kaldan itatoa huduma katika ngazi zifuatazo mbaimbali ikiwemo Childcare/Daycare kwa watoto kuanzia mwaka mmoja na kuendelea, Nursery, Msingi kuanzia Darasa la Kwanza hadi la Tatu.





