Na John Bukuku- Dar es salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ameonya na kuelezea wasiwasi juu ya kuendelea kuenea kwa chuki katika jamii kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea jijini Dar es Salaam, ikiwamo kuchomwa moto vituo vya mafuta na uharibifu wa mali za wananchi.
Akizungumza na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika kikaokazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa JNICC, Chalamila amesema kuwa matukio ya uharibifu yamewaathiri hata wananchi wa hali ya chini bila kuwa na kosa lolote.
Aidha, Chalamila amebainisha kuwa hivi karibuni kumeibuka madai kuwa vituo vinavyoteketezwa moto ni mali ya viongozi mbalimbali wa kitaifa, hatua iliyochochea hisia na kuchangia baadhi ya wananchi kuingia barabarani na kufanya vurugu.
Amesema kuwa siku ya tukio sehemu ya vijana walionekana wakiwa na minyororo ya kubomoa milango na wengine wakichoma matairi katika eneo la Kimara Mwisho, tofauti na maandamano aliyowahi kushiriki awali yaliyotokea kutoka Mbezi hadi mjini ambayo hayakuhusisha silaha wala uharibifu.
Chalamila amesema kuwa mjadala muhimu unaopaswa kuangaliwa na jamii ni kujua nani alianza kufanya uharibifu huo, kama ni waandamanaji au chombo kingine, ili kupata ukweli wa matukio. Amebainisha kuwa hata askari hupata msongo wanapoona raia au wenzao wakipoteza maisha katika mazingira ya vurugu.
Aidha, amebainisha kuwa hotuba ya Rais ilisisitiza umuhimu wa msamaha na kutafuta suluhu, akimnukuu Yesu katika kitabu cha Luka kuhusu kuwasamehe wasiojua wafanyalo. Amewataka wadau kuangalia malalamiko ya wananchi kwa upana wake na kuyafanyia kazi badala ya kuendeleza chuki.
Aidha, amesema kuwa serikali imeunda tume maalumu kukusanya taarifa kutoka kwa mtu yeyote ili kutoa mapendekezo ya hatua sahihi za kuchukua baada ya matukio hayo, na kwamba tume hizo huwa na uwezo mpana wa kuchunguza na kuchambua taarifa.





