Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akizungumza leo, Desemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall.

Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Mhandisi Dkt. Richard Joseph Masika akizungumza leo, Desemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall.

Mkuu wa DIT, Prof. Preksedis Marco Ndomba, akizungumza leo, Desemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee Hall.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda akikagua ubunifu za wanafunzi wa DIT katika Mahafali ya 19.


Wanataaluma wa DIT wakiwa katika maandamano ya mahafali ya 19


Wahitimu wa fani mbalimbali wakiwa katika mahafali ya 19

…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeongeza fursa za mafunzo na elimu ya ufundi stadi pamoja na kusimamia ubora wa elimu ili kumuandaa Mtanzania kuwa na maarifa, stadi na mtazamo chanya utakaomwezesha kuchangia katika maendeleo endelevu ya Taifa.
Akizungumza leo, Desemba 5, 2025 jijini Dar es Salaam, katika Mahafali ya 19 ya Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda amesema kuwa Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia imewekeza jumla ya dola milioni 90 za Marekani. Kati ya fedha hizo, Kampasi ya Dar es Salaam imejenga Kituo cha Umahiri cha Kikanda cha Mafunzo ya TEHAMA (RAFIC) kwa gharama ya dola milioni 19.75, huku Kampasi ya Mwanza ikiwekeza dola milioni 18.75 kujenga Kituo cha Umahiri cha Uchakataji wa Bidhaa za Ngozi (CELPAT).
Amesema Serikali imeongeza kasi ya kutoa ujuzi kwa vijana ili kuwawezesha kuajiriwa au kujiajiri kupitia miradi inayofadhiliwa na mashirika na mataifa mbalimbali kwa lengo la kukuza umahiri nchini.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa ili wataalam wapate uzoefu unaoendana na mahitaji ya kikanda na kimataifa.
“Niwapongeze DIT kwa ushirikiano wenu na taasisi za elimu kutoka nchi mbalimbali ikiwamo China, Ethiopia, Urusi, Ufaransa, Uganda, Uturuki, Kenya, Korea, Marekani, Italia, Ireland, Cyprus na Afrika Kusini,” amesema Prof. Mkenda.
Katika hatua nyingine, amewasisitiza wahitimu kuwa na moyo wa kujiajiri na kuvuka changamoto watakazokutana nazo, kwani jamii ina matarajio makubwa kutoka kwa mafundi sanifu na wahandisi waliobobea DIT.
Amesema anatarajia wahitimu kuonesha umahiri na kuwa mfano bora katika maeneo yao ya kazi ili kulitangaza vyema taasisi hiyo na kuwajengea matumaini walezi, wazazi na walimu.
Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Mhandisi Dkt. Richard Joseph Masika, amewataka wahitimu kutumia maarifa yao kutoa huduma bunifu na kitaalamu ili kukidhi mahitaji ya jamii.
Amesisitiza pia umuhimu wa bidii, uaminifu na nidhamu, vigezo ambavyo waajiri wengi huzingatia wanapotafuta wataalam.
Naye Mkuu wa DIT, Prof. Preksedis Marco Ndomba, amesema wahitimu walinufaika na ziara za mafunzo viwandani ambazo zimewajengea ubunifu na kuwasaidia kuanzisha kampuni zao.
Amewapongeza kwa kuzalisha bunifu zenye viwango, akibainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya taasisi na wadau mbalimbali wakiwemo Tanga Cement, Azam, TBS, TANESCO, TRC na TCRA.
Kwa upande wao, wahitimu wameushukuru uongozi wa DIT kwa kuwapatia elimu bora itakayowasaidia kufikia malengo yao na kuchangia maendeleo ya Taifa.




