Na Meleka Kulwa- Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameongoza kikao maalumu cha maombi kilichowakutanisha viongozi wa dini katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na kusisitiza umuhimu wa kuendeleza amani wakati huu ambao kumekuwepo na taharuki katika maeneo mbalimbali.
Kikao hicho kimefanyika Desemba 5,2025 Jijini Dodoma
Bi. Senyamule amesema kuwa kumekuwepo na watu wachache wanaotamani uvunjifu wa amani, hivyo wananchi wanaopenda amani wanapaswa kuendelea kupaza sauti na kuonesha umoja katika siku tatu za maombi zilizotangazwa na Serikali kuanzia Desemba 7 hadi 9. Amesema kuwa huu si wakati wa kulala usingizi, bali ni kipindi cha wananchi kushikana na kuzungumza lugha ya amani ili kutimiza wajibu wao wa kulinda utulivu wa taifa.
Aidha amebainisha kuwa viongozi wa dini wana nafasi muhimu katika kuhamasisha umoja, kuimarisha maelewano na kutuliza mioyo ya wananchi, hasa kutokana na taarifa zinazodai uwezekano wa machafuko kuelekea Desemba 9. Ameongeza kuwa maombi yanapaswa kupewa kipaumbele ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na mshikamano.
Pia, Senyamule amesema kuwa wananchi wanatakiwa kuendelea kumuomba Mungu ili Tanzania ibaki kuwa nchi ya utulivu, upendo na mshikamano, akisisitiza kuwa si busara kusubiri tu kitakachotokea tarehe 9, bali kila mmoja ana wajibu wa kuchukua hatua sasa ili kuhakikisha kesho kunakuwa na salama.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ambao walitumia nafasi hiyo kuiombea nchi na kuwasisitiza wananchi kupuuza taarifa zinazoweza kuchochea uvunjifu wa amani.





