Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo, hususan vijana, kutumia kikamilifu fursa zilizopo katika sekta ya kilimo kwa kujikita kwenye kilimo biashara chenye tija, ili kuongeza kipato, kuboresha usalama wa chakula na kuchochea ukuaji wa viwanda.
Akizungumza katika Tamasha la Soka na Kilimo Biashara Gonja Inawezekana lililofanyika katika Tarafa ya Gonja, Mhe. Mgeni alisema kilimo biashara ni njia madhubuti ya kuinua uchumi wa kaya, hasa kupitia mazao ya tangawizi, parachichi na kahawa ambayo yameonekana kustawi vizuri katika maeneo ya wilaya hiyo.
“Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uzalishaji na usafirishaji wa mazao kupitia maboresho ya miundombinu, huduma za ugani na matumizi ya teknolojia za kisasa. Ni jukumu letu wananchi kuyatumia kikamilifu mazingira haya ili kuongeza tija na faida katika kilimo,” alisema Mhe. Kasilda.
Aidha, aliwaagiza maafisa kilimo kuhakikisha wanawafikia wakulima katika vijiji na kata zote kwa kuwapatia elimu, maarifa na mbinu zitakazowawezesha kuzalisha kwa ufanisi zaidi.
Kwa upande wake, mwanzilishi wa tamasha hilo ambaye pia ni Afisa Tarafa ya Gonja, Bi. Rhobi Stephano, alisema tamasha hilo limeanzishwa ili kuinua kipato cha wananchi kupitia mazao ya kibiashara, pamoja na kuwaelimisha vijana kuachana na vitendo visivyofaa kama matumizi ya dawa za kulevya, ulevi kupita kiasi na wizi, na badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji mali.
Tamasha hilo lilikuwa na kaulimbiu isemayo “SOKA NA KILIMO BIASHARA GONJA INAWEZEKANA” ambalo limeangazia zaidi mazao ya tangawizi, parachichi na kahawa, likiwalenga vijana wa kata za Vuje, Bombo, Mtii na Lugulu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza uchumi wa eneo hilo kupitia kilimo chenye tija.





