Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imetoa taarifa kuhusu hatua za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na Jumuiya ya Kimataifa, kufuatia mazungumzo yaliyofanyika leo Ijumaa, tarehe 28 Novemba 2025, kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), na Jumuiya ya Wanadiplomasia (Diplomatic Corps) nchini.
Mkutano huo, ambao ni wa kwanza kufanyika tangu kuundwa kwa Serikali mpya ya Awamu ya Sita kipindi cha pili baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, uliangazia ajenda mbalimbali zinazohusu mahusiano ya kimataifa pamoja na mwenendo wa hali ya nchi.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema, Waziri Kombo aliwahakikishia Mabalozi hao kuwa Tanzania itaendeleza ushirikiano na nchi wanazotoka pamoja na mashirika wanayoyawakilisha, akibainisha kuwa dhamira ya washirika hao kuendelea kufanya kazi na Tanzania ni kielelezo cha ukomavu wa diplomasia na uimara wa uhusiano wa muda mrefu wa maendeleo.
Aidha, Serikali ilitumia mkutano huo kuwapatia Mabalozi taarifa kuhusu hali ya uchaguzi uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025 na changamoto zilizojitokeza. Pamoja na vurugu zilizotokea, Serikali imeeleza hatua ilizochukua ikiwa ni pamoja na kurejesha utulivu, kulinda maisha na mali za wananchi, na kuhakikisha huduma muhimu na shughuli za kiuchumi zinaendelea kama kawaida. Waziri pia alifafanua kuhusu Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa na Rais kwa lengo la kuchunguza matukio hayo na kuandaa mapendekezo ya hatua za kuimarisha mifumo ili kuzuia kurudiwa kwa matukio kama hayo.
Waziri Kombo alisisitiza kuwa Tanzania imepitia kipindi kigumu ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika historia yake, lakini sasa Taifa linaingia katika hatua ya kujenga maridhiano, kuponya majeraha ya kijamii na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Alibainisha kuwa Serikali inafanya tathmini ya kina na itaendelea kuchukua hatua muhimu kupitia majadiliano, uwajibikaji na uimarishaji wa taasisi.
Katika maelezo yake, Waziri aliwataka wadau wa kimataifa kutoa nafasi kwa Tanzania kukamilisha uchunguzi unaoendelea, akionya kuwa baadhi ya matamko yanayotolewa yanaweza kuingilia au kupotosha mchakato huo. Alisisitiza umuhimu wa kuheshimu uhuru wenye mipaka na uwajibikaji.
Kuhusu maazimio ya Bunge la Umoja wa Ulaya, Waziri Kombo alisema Tanzania imeyapokea na kuelekeza Balozi wake mjini Brussels kuendelea na mashauriano ya kidiplomasia na taasisi za Umoja wa Ulaya pamoja na wadau husika ili kuimarisha ushirikiano na kulinda maslahi ya Taifa.




