Mkuubwa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile akizungumza mara baada ya kufika kwenye daraja lililosombwa na maji
Andrea Siame kutoka katika kijiji cha Sakalilo akizungumza adha wanayokutana nayo baada ya daraja la sakalilo kusombwa na maji ya mvua.
……………….
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Wananchi wa Kijiji cha Sakalilo kata ya Ilemba wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa wameeleza kukumbwa na changamoto kubwa za usafiri na mawasiliano kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha na kusababisha daraja la sakalilo kusombwa na maji
Andrea Siame mkazi wa kijiji cha sakalilo amesema hali hiyo imewazuia kufanya shughuli za uzalishaji na kuwafanya washindwe kuvuka kwenda katika maeneo mbalimbali.
“Mvua hizi zimekuwa kikwazo kikubwa hasa pale barabara zinapokatika jamii hukosa huduma muhimu za kijamii na kiuchumi ” amesema Siame.
Kufuatia hali hiyo Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile amelitaka jeshi la zimamoto na uokoaji kuweka kambi katika daraja la sakalilo linalounganisha vijiji vya sakalilo,lyanza, Kasteka, ilemba A, na ilemba B kwa lengo la kuokoa maisha ya watu.
Hatua hiyo imekuja baada ya mvua zinazoendelea kunyesha kusababisha kuharibika kwa miundombinu ya daraja hilo kusombwa na maji na ambalo hutegemewa na wakazi wa vijiji hivyo.
Akizungumza leo Novemba 24,2025 Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga amesema usiku wa kuamkia leo mvua kubwa imenyesha ambayo imeleta madhara makubwa na wananchi kushindwa kupita katika daraja hilo ambalo limekata mawasiliano kati ya kata ya Muze na mtowisa .
Amesema mwanzoni waliweka vizingiti vya miti ili kuwasaidia wananchi kuweza kupita kwa urahisi lakini vimesombwa na maji.
Amesema eneo hilo liliathirika na mvua za mwaka 2023/2024/2025 na hivyo kulitaka jeshi la zimamoto na uokoaji kuweka kambi kwa lengo la kuimarisha uokoaji na kutoa elimu kwa wananchi kuacha tabia ya kuogolea katika eneo hilo hasa watoto na kuhama kwenye maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Pia amemtaka polisi kata akishirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya kuweka zuio la wananchi kutopita katika daraja hilo hasa nyakati za jioni lengo likiwa ni kuchukua tahadhari juu ya maafa hayo.
Aidha Dc Chirukile amesema nyumba zaidi ya 38 zimebomoka kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na kuwaacha wakazi wa kata ya Mpui bila makazi huku wakihifadhiwa kwa ndugu na jamaa zao na wananchi wengine watatu kujeruhiwa katika maafa hayo na wamepatiwa matibabu na kuruhusiwa kuendelea na shughuli zao.
Sambamba na hilo pia amewataka watendaji ,wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuwaelimisha wananchi kuhama mabondeni ,kupanda ukoka ,na matete kwa lengo la kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Naye mtendaji wa kata ya Ilemba Happy Samweli amesema watasimamia zoezi la wananchi kuhama katika maeneo hatarishi karibu na daraja hilo ambalo limekuwa ni bonde kubwa na maji yanayopita kwa kasi kubwa na kusababisha mmomonyoko wa ardhi unaosogea mpaka kwenye makazi ya watu.
“Kuna baadhi ya wananchi wameanza kuhama lakini wengine bado wanasuasua na wameanza kulima kwenye vyanzo vya maji tutawaelimisha kwa kuwa usalama ni mdogo na hizi mvua ni za mwanzo tu” amesema afisa mtendaji
“Serikali inaendelea kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuwa salama kwa kutoa tahadhari na kuweka vizuizi wakati wakala wa barabara nchini (TANROADS) wakijipanga kuikabili barabara hiyo.”amesisitiza Chirukile





