NA DENIS MLOWE ,IRINGA
MBUNGE wa Iringa Mjini, Fabian Ngajilo, baada ya kuapishwa rasmi kuwa mwakilishi wa wananchi wa Jimbo hilo amepokelewa Iringa Mjini kwa shangwe na hamasa kubwa na wananchi waliojitokeza katika ofisi za CCM mkoa.
Ngajilo aliyechaguliwa kwa kishindo katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29 mwaka kwa zaidi ya asilimia 90 amewasili mjini Iringa leo majira ya saa nne na nusu na kupokelewa na msafara mkubwa kutoka km 7 eneo la Kihesa hadi makao ya ccm mkoa wa Iringa.
Akiwahutubia wananchi Ngajilo ameanza kwa kutoa pongezi za kipekee kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa busara wa kuanzisha Tume ya Maridhiano akisema ni hatua muhimu katika kuimarisha umoja, utulivu na mustakabali wa Taifa.
Ngajilo amesema Tume hiyo inaonyesha dhamira njema ya Rais Samia katika kuwaleta watanzania pamoja.
Aidha Ngajilo aliwashukuru wananchi wa Iringa Mjini kwa kumuamini na kumpa kura za kutosha, pamoja na kura nyingi alizopata Rais Samia katika Jimbo hilo.
Amesema heshima aliyopewa ni deni atakalolipa kwa kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana na makundi yote katika jamii.
Alisema kuwa ameanzisha dawati mbalimbali ambazo zitakuwa maalum kusikiliza kero za wananchi ambapo kutakuwa na dawati la wanawake, siasa na vijana ambapo watapeleka kero zao na kuziletea ufumbuzi.
Ameahidi kuanzisha Dawati la Wanawake, pamoja na ofisi shirikishi kwa viongozi wote wakiwemo wa serikali za Mitaa, Mabalozi na wananchi wa kada zote, ili kuhakikisha changamoto zao zinasikilizwa na kutatuliwa kwa wakati.
Mbunge huyo ameweka msisitizo mkubwa kwenye amani, akisema bila amani hakuna maendeleo na kwamba Rais Samia ndiye kinara wa kudumisha utulivu nchini huku akitoa pole kwa wale wote waliopitia changamoto kipindi cha vurugu za uchaguzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iringa Mjini, Said Rubeya amempongeza Ngajilo kwa kupata zaidi ya asilimia 94 ya kura akiwataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano ili azma ya maendeleo kwa Jimbo la Iringa Mjini itimie.





