Na.Alex Sonna-Dodoma,
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amezindua rasmi mpango wa ugawaji wa majiko ya kupikia kwa umeme kwa bei ya ruzuku kwa wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), hatua inayolenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Agosti 14,2025 jijini Dodoma, Dkt. Biteko amesema mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira. Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2022, ni asilimia 4.2 pekee ya Watanzania wanaotumia umeme kwa kupikia, kiwango ambacho alisema ni kidogo kulingana na idadi ya Watanzania.
Kwa maelezo yake, historia na mitazamo potofu kuhusu gharama za kupikia kwa umeme imechangia matumizi yake kuwa madogo. Alifafanua kuwa utafiti wa TANESCO umebaini majiko janja ya umeme yanaweza kutumia chini ya uniti moja ya umeme kuandaa mlo mmoja, sawa na gharama ya chini ya shilingi 352.
Kupitia mpango huu, TANESCO kwa kushirikiana na Modern Energy Cooking Services (MECS) chini ya Serikali ya Uingereza, imenunua zaidi ya majiko 11,000 yatakayogawiwa kwa wafanyakazi wake kupitia mfuko wa mzunguko (revolving fund).
Aidha Wafanyakazi hao wanatarajiwa kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jamii.
Dkt. Biteko amesema kuwa baadaye mpango huo utawahusisha pia wateja wa TANESCO watakaopewa majiko na kulipa kidogo kidogo kupitia bili za umeme (On bill financing), hatua inayotarajiwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma hiyo nchini.
Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema ugawaji huo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia unaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisisitiza kuwa Wizara na taasisi zake zinajipanga kutekeleza ajenda hiyo kwa vitendo.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amemshukuru Rais Samia kwa kuimarisha miradi ya umeme mkoani humo, ikiwemo miradi ya vijijini yenye thamani ya shilingi bilioni 214.3, na kuendeleza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kama vile gesi, umeme wa jua na upepo.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, alisema mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kufikia lengo la serikali la kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Mwakilishi wa MECS, Charles Barnabas, alisema majiko hayo yanatumia kiasi kidogo cha umeme na ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya “Pika Smart”, inayolenga kuelimisha wananchi juu ya manufaa na unafuu wa kupikia kwa kutumia nishati safi.