Kaimu Meneja wa TMD Kanda ya Ziwa Mashariki,Aggrey Muhabuki akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kwenye maonesho ya Nanenane Jijini Mwanza
Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Wafugaji wametakiwa kuepuka matumizi ya dawa kwenye mifugo zinazo nenepesha wanyama wao ambazo zinaweza kuleta madhara kwa binadamu baada ya kula vyakula vyake.
Wito huo umetolewa Jana Jijini Mwanza na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki, Aggrey Muhabuki alipokuwa akizungumza na Waandishi Habari katika maonesho ya Nanenane Jijini Mwanza.
Alisema matumizi ya dawa hizo ambazo zimekuwa zikitolewa kwa ng’ombe, mbuzi, kuku na wanyama wengine zina viambata vya sumu ambavyo vina madhara kwa binadamu.
Muhabuki alisema matumizi sahihi ya dawa na vitendanishi ni muhimu kuzingatiwa na wauzaji, wasambazaji, wafugaji na wavuvi katika kulinda afya ya binadamu.
Alisema kupitia maonesho ya Nanenane wameweza kutembelea vibanda mbalimbali na kuzungumza nao juu ya kujihadhari na matumizi ya dawa ambazo siyo sahihi.
Aidha Muhabuki alisema kuwa madhara yanayosababishwa na dawa hizo zisizo sahihi zinaweza kuwa kwenye nyama, maziwa na mayai hivyo mtu anapokula zinaweza kumuathiri.
Alisema wataendelea kuwatembelea wauzaji wa dawa za mifugo mara kwa mara kama ilivyo utaratibu wao wa kawaida kwa ajili ya kufanya ukaguzi.