Na .Alex Sonna-Dodoma
WAFUASI na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamejitokeza kwa wingi leo nje ya Jengo la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) jijini Dodoma, wakimsubiri kwa hamu Mgombea Urais wa chama hicho, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Samia anatarajiwa kuwasili katika jengo hilo akiongozana na Mgombea Mwenza, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kwa ajili ya kuchukua fomu ya uteuzi wa kugombea nafasi ya Urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Wafuasi hao wameonekana wakiwa na mavazi ya chama, mabango, bendera pamoja na nyimbo za kuhamasisha, ikiwa ni ishara ya kuonyesha mshikamano na kumuunga mkono mgombea wao.
Zoezi la uchukuaji fomu linafanyika kwa mujibu wa ratiba rasmi ya Tume ya Uchaguzi, ambapo vyama mbalimbali vya siasa vinawasilisha majina ya wagombea wao kwa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.