Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe. Nurdin Babu (kushoto), akimkabidhi kombe na cheti cha mshindi wa kwanza Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Prof. Maulilio Kipanyula (kulia), baada ya taasisi hiyo kuibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Taasisi za Elimu ya Juu wakati wa kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini yaliyofanyika tarehe 8 Agosti 2025 katika viwanja vya Themi Njiro, Jijini Arusha.




Mgeni rasmi, Mhe. Nurdin Babu, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, akiongozana na mwenyeji wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenani Kihongosi, wakitembelea banda la Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wakati wa kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, yaliyofanyika katika viwanja vya Themi Njiro, Jijini Arusha, tarehe 8 Agosti 2025.


Makamu Mkuu wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), Prof. Maulilio Kipanyula, akiwa ameshika kikombe cha ushindi wa kwanza katika picha ya pamoja na washiriki na wabunifu wa taasisi hiyo, katika banda la maonesho wakati wa kilele cha Maonesho ya Nanenane Kanda ya Kaskazini, yaliyofanyika katika viwanja vya Themi Njiro, Jijini Arusha, tarehe 8 Agosti 2025.
Na.Mwandishi Wetu.
Ni wazi kuwa ubunifu na utafiti vina nafasi kubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo nchini na Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) imethibitisha hilo kwa vitendo baada ya kushinda tuzo ya mshindi wa kwanza katika kipengele cha Taasisi za Elimu ya Juu kwenye kilele cha Maonesho ya 31 ya Kilimo, Mifugo na Sherehe za Wakulima (Nanenane) kwa Kanda ya Kaskazini, yaliyofanyika Agosti 8, 2025.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Makamu Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Maulilio Kipanyula, alisema mafanikio hayo ni matokeo ya kazi ya miaka mingi ya kufanya tafiti ,bunifu zenye lengo la kuibua suluhisho kwa changamoto za wakulima na wafugaji nchini.
“Tumejipanga kuifanya NM-AIST iwe taasisi ya ubunifu wa kweli, bidhaa na teknolojia tunazozalisha ni majibu ya changamoto ambazo jamii inakabiliana nazo kila siku siyo vitu vya maabara tu,” alisema Prof. Kipanyula.
Alifafanua kuwa maonesho hayo yamefungua milango kwa ushirikiano mpya na wadau mbalimbali waliovutiwa na teknolojia kutoka kwa taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja na kampuni, mashirika ya maendeleo na hata watu binafsi wanaotaka kushirikiana kwenye uzalishaji wa teknolojia hizo.
“Tumekuwa kinara kitaifa kwa kusajili tafiti nyingi kuliko taasisi nyingine za elimu ya juu, lakini si tafiti za vitabuni bali tafiti zenye suluhisho,” aliongeza Prof. Maulilio Kipanyula
Katika banda la NM-AIST teknolojia na bunifu mbalimbali zilionyeshwa ikiwemo:Chanjo ya samaki,Ufugaji wa funza lishe kwa chakula na mbolea,Mbinu za kuongeza tija kwa wafugaji,Dawa ya kusindika ngozi kwa kutumia maganda ya korosho,Mtambo wa kuchakata taka na kuzalisha mbolea asilia.
Kwa mujibu wa Prof. Kipanyula, taasisi hiyo inakwenda mbele zaidi kwa kuhakikisha watafiti wake wanazalisha maarifa yanayoweza kubadilishwa kuwa bidhaa halisi na huduma za moja kwa moja kwa wananchi.