Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipewa maelezo na mwanafunzi wa ubunifu wa nguo na teknolojia ya nguo, Sophia Mohammed, wakati alipokagua karakana ya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nandagala, wilayani Ruangwa. Kushoto ni Msajili wa Chuo VETA Ruangwa, Mohammed Salum.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa wazazi na walezi kote nchini kuhakikisha wanawapeleka vijana wao kupata mafunzo ya ufundi stadi yanayoratibiwa na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawezesha kupata ujuzi utakaowasaidia kujiajiri na kuchangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kukagua karakana za kujifunzia zilizopo katika Chuo cha VETA wilayani Ruangwa mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha miundombinu ya vyuo vya ufundi stadi pamoja na kuratibu programu za mafunzo ili kuhakikisha vijana wanapata stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira la sasa na baadaye.
“Serikali inayo dhamira ya dhati ya kuhakikisha vijana wa Kitanzania wanakuwa na ujuzi. Mafunzo ya VETA na yale yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu yanawawezesha vijana wetu kuajiriwa au kujiajiri wenyewe, na hii ni hatua kubwa ya maendeleo kwa familia zao na Taifa kwa ujumla,” alisema Waziri Mkuu.
Katika mazungumzo yake na baadhi ya wanafunzi alipokuwa akitembelea karakana chuoni hapo, Mheshimiwa Majaliwa alifurahishwa na namna ambavyo programu hizo za mafunzo zimekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wanafunzi hao.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Mohamed Salum alisema kuwa VETA Ruangwa inaendelea kufanya maboresho mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa kozi zinazotolewa ili kwenda sambamba na mahitaji ya soko la ajira. Alitaja jitihada zinazofanyika kuwa ni pamoja na mpango wa uanzishwaji wa fani mpya na uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kufundishia.
Naye Mwanafuzi mnufaika wa programu ya mafunzo ya Ofisi wa Waziri Mkuu Maganga Salum amesema kuwa kabla ya kujiunga chuoni hapo hakuwa na ujuzi wowote, lakini kupitia mafunzo hayo sasa anaweza kufanya kazi za ufundi na ana matumaini makubwa ya kujiajiri mara baada ya kuhitimu. “Tumeiva na sasa tupo tayari kwenda kufanya kazi.”
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu pia alitembelea eneo linalojengwa hosteli kwa ajili ya timu ya mpira wa miguu ya Namungo sambamba na kukagua uwanja wa michezo wa Kassim Majaliwa uliopo Ruangwa ambao unatarajiwa kuwekwa viti katika majukwa.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipewa maelezo na mwanafunzi wa ubunifu wa nguo na teknolojia ya nguo, Sophia Mohammed, wakati alipokagua karakana ya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nandagala, wilayani Ruangwa. Kushoto ni Msajili wa Chuo VETA Ruangwa, Mohammed Salum.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akipewa maelezo na mwanafunzi wa ufundi wa magari daraja la pili Veronica Petro, wakati alipokagua karakana ya Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nandagala, wilayani Ruangwa. Katikati ni Msajili wa Chuo VETA Ruangwa, Mohammed Salum.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Nandagala, wilayani Ruangwa, baada ya kukagua karakana za Chuo hicho.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua hosteli zinazojengwa kwa ajili ya timu ya ya mpira wa miguu ya Namungo wilayani Ruangwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua miundombinu ya uwanja wa michezo wa Kassim Majaliwa wilayani Ruangwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)