Meneja wa Chama cha akiba na mikopo Mahanje Saccos Kassim Masengo,akizungumza jana ofisini kwake kuhusu mafanikio ya chama hicho katika kipindi cha miaka minne cha Serikali ya awamu ya sita.

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha akiba na mikopo Mahanje Saccos Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma wakipata huduma mbalimbali za mikopo na fedha kwenye Chama chao.

Meneja wa Chama cha akiba na mikopo Mahanje Saccos Kasim Masengo kulia na baadhi ya wakulima ambao ni wanachama wa chama hicho wakimsikiliza Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Madaba Wilayani Songea Sadam Fupi aliyetembelea moja ya shamba la mkulima wa mahindi katika kijiji cha Madaba

Mkulima wa zao la mahindi ambaye ni Mwanachama wa Chama cha akiba na mikopo Mahanje Saccos ambaye hakufahamika jina lake mara moj kushoto,akimuonyesha Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Madaba Wilayani Songea Sadam Fupi sehemu ya shehena ya mahindi aliyozalisha katika msimu wa kilimo 2024/2025,katikati Meneja wa Mahanje Saccos Kasim Masengo.
Na Mwandishi Wetu,Madaba
CHAMA cha akiba na mikopo Mahanje Saccos kilichopo katika Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma,kimetoa mikopo yenye thamani ya Sh.milioni 900 kwa wanachama wake katika kipindi cha miaka minne.
Meneja wa Chama hicho Kassim Masengo alisema,wanachama wametumia mikopo hiyo kwenye biashara,ujenzi wa nyumba bora na kilimo hususani zao la mahindi ambalo ni uti wa mgongo na uchumi kwa wananchi wa Halmashauri ya Madaba na Mkoa wa Ruvuma.
Masengo alisema,Mahanje Saccos ilianzishwa kwa madhumuni ya kuwasaidia wakulima ili kupata huduma mbalimbali ikiwemo mikopo ya fedha kwa wanachama wake ambao wako 1,733.
Masengo alisema, Mahanje Saccos inashughulika na huduma ya kutunza fedha za wanachama ambao wanaitumia Saccos hiyo kama Benki kwa kuweka na kuchukua fedha pamoja na kutoa huduma za mikopo.
Kwa mujibu wa Masengo,Mahanje Saccos inatoa huduma kwenye kata tatu ambazo ni Mahanje,Lituta na Mkongotema zenye vijiji 8 na tangu ilipoanzishwa wanachama wanafurahi kupata mikopo yenye masharti nafuu na riba ndogo.
“lakini Mahanje Saccos haijaishia kutoa huduma za kifedha tu,inatoa mafunzo mbalimbali juu ya matumizi sahihi ya fedha na elimu kwa wakulima namna ya uzalishaji wa mazao bora na imeajiri mtaalam wa kilimo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima ambao ni wanachama”alisema Masengo.
Alisema, asilimia kubwa ya wakulima wake wanajihusisha na kilimo cha zao la mahindi,maharage na mpunga na zao la mahindi soko kubwa ni la Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA)Kanda ya Songea na kwa muda wa miaka minne wameuza zaidi ya tani 90.
Ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuwapatia wanachama nafasi ya kuuza mahindi kwenye ushirika, hivyo kuwawezesha kurudisha mikopo kwa wakati ikilinganisha na miaka ya nyuma ambapo wakulima hawakupata soko la uhakika badala yake waliuza mahindi kwa walanguzi kwa bei ndogo.
Ameishukuru ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Madaba, kupitia idara ya ushirika kwa usimamizi wa karibu uliosaidia Chama kuendelea kuwa imara na kuwa na nguvu kubwa katika kuwasaidia wanachama wake.
“tumeanza kutoa mikopo ya afya maarufu mikopo ya dharura ambayo ikitokea mwanachama anaugua tunampa mkopo mwingine aweze kupata matibabu na akishapona aweze kuendelea na shughuli zake za uzalishaji, chama kinatambua bila mwanachama kuwa na afya njema hawezi kushiriki kikamilifu kwenye uzalishaji na urudishaji wa mikopo.
Alisema,kwenye suala la Bima ya afya wamekuwa mabalozi wazuri wa Serikali na wanaendelea kuwaelimisha wanachama waweze kukata na kujiunga na bima ya afya kwa wote kwa kuwa mwanachama mwenye afya njema atakuwa na uwezo wa kuzalisha na Mahanje Saccos itaendelea kuwa imara.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Madaba Sadam Fupi alisema, Halmashauri imekuwa bega kwa bega na vyama vya ushirika ili viweze kufuata sheria na kanuni zilizowekwa kwa ajili ya kuhakikisha vinakuwa na vinatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha alisema,Halmashauri imekuwa inasimamia soko la mazao kwa kuhakikisha mazao yanayozalishwa yanauzwa kwenye mfumo wa stakabdhi ghalani kwa njia ya minada na soko la Serikali kupitia wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula(NFRA) ambayo inanunua mahindi kupitia vyama vya ushirika.
Alisema,kwenye vyama vya ushirika kila mwaka kuna mgao unaotolewa kwa ajili ya wakulima kuuza mahindi licha ya kutokuwa sehemu ya mazao yanayotakiwa kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani lakini Serikali imeweka upendeleo kwa wakulima kuuza mahindi kupitia Amcos zao.
Alisema,kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani wakulima wamenufaika saana kwa kupata bei nzuri ambayo imesaidia sana kurudisha gharama za uzalishaji ikilinganisha na bei inayotolewa na wafanyabiashara binafsi ambayo ni Sh.450 badala ya Sh.700 inayotolewa na Serikali.
Fupi,ameipongeza Serikali kuwaletea wakulima bei nzuri na kununua mahindi kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani ambao umewanufaisha wakulima na wanacahama wa vyama vya msingi vya ushirika.
Mwanachama wa Chama hicho Winfrid Mfikwa alisema,tangu alipojiunga na Saccos hiyo ametapa faida kubwa ikiwemo kudhibiti matumizi holela ya fedha zake na uhakika wa ulinzi wa fedha anazopata kutokana na shughuli zake za kilimo.
Amewataka wakulima ambao bado hawajajiungana Chama hicho kuhakikisha wanatumia fursa hiyo kujiunga kwenye Saccos ili waweze kunufaika na furasa zilizopo ikiwemo mikopo kwa ajili ya kilimo ili waweze kuzalisha kwa tija.
Mkulima wa mahindi wa kijiji cha Madaba Hamis Malua,amepongeza mpango wa Serikali wa kutoa pembejeo za ruzuku kwa wakulima kwani umesaidia sana wakulima kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa mazao mashambani.
Alisema,awali walipata shida kwenye uzalishaji kwani upatikanaji wa mbolea ulikuwa mgumu kwa sababu mbolea ilikuwa inauzwa kwa bei kubwa ambayo wakulima wengi walishindwa kumudu gharama zake.