NA DENIS MLOWE IRINGA
TAASISI ya Swiss Contact inatarajia kutekeleza mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) unaofadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi kuweza kuwafikia vijana zaidi ya 3000 kutoka kada mbalimbali mkoani Iringa.
Akizungumza na wanahabari kuhusu mradi huo,Mratibu wa Mafunzo ya Kiufundi kwa Vijana kutoka Swiss Contact, Jonathan Ngonyani, alisema taasisi hiyo imezindua wiki ya maonyesho ya ajira na ujuzi kwa vijana yanayofanyika kuanzia Julai 21 hadi 27, yakilenga kuwaunganisha vijana na fursa mbalimbali za ajira na mafunzo stadi.
Alisema kuwa kupitia mradi huo wanataka vijana nchini kutumia ipasavyo fursa za ujuzi katika fani mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine badala ya kusubiri ajira kutoka serikalini
Ngonyani alisema kuwa maonyesho haya ya Ujuzi, Fani na Ajira kwa Vijana 2025 yanafadhiliwa na Ubalozi wa Uswisi nchini Tanzania na kuandaliwa na shirika la Tourism Innovation Hub kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Swisscontact Tanzania.
Alisema malengo yake makubwa ni Kuongeza ufahamu kwa vijana juu ya ujuzi unaohitajika katika ulimwengu wa kazi na ajira.
Aidha kuwezesha vijana kuwasiliana na kujadili ana kwa ana na wataalamu, wafanyabiashara na waajiri mbalimbali wenye uzoefu.
Vilevile aliongeza kuwa lengo ni Kutoa nafasi kwa vijana kuelewa namna taasisi za kifedha zinavyofanya kazi na namna ambavyo vijana wanaweza kuzitumia katika kukuza mitaji yao.
Alisema kuwa maonyesho hayo yatawezesha vijana kuelewa namna mradi wa Skills for Employment Tanzania (SET) ulio chini ya Ubalozi ya Uswisi unavyofanya kazi ya na kuchangia katika ukuzaji wa ujuzi nchini Tanzania.
Kwa niaba ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Afisa Atilio Mganwa alisisitiza kuwa vijana ni kundi kubwa na nguvu kazi ya taifa, hivyo kushiriki kwao kikamilifu katika maonyesho hayo ni hatua muhimu ya kupunguza utegemezi katika jamii.
Naye Mwakilishi wa Vyuo Vikuu Mkoani Iringa ambaye pia ni mbunifu kutoka Chuo Kikuu cha Iringa, Eric Kisanga, aliwataka vijana kutumia vyema jukwaa hilo kujitangaza na kuonyesha uwezo wao.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Madereva wa Bajaji Manispaa ya Iringa, Ally Seleman, aliwahimiza vijana wenzake kujitokeza kwa wingi kushiriki maonyesho hayo amesema, hiyo ni nafasi ya kipekee kwa vijana kuonyesha vipaji na kupata mitandao ya kibiashara.
Maonyesho ya Ujuzi, Fani na Ajira kwa Vijana 2025 yatafanyika katika viwanja vya wazi vya Mwembetogwa ikitanguliwa na shughuli za kijamii kwa kuanzia Jumatatu tarehe 21 Julai — Alhamisi tarehe 24 Julai, 2025.
Maonyesho hayo yanaratibiwa na Swiss Contact kupitia mradi wa Skills for Employment Tanzania kwa ufadhili wa Ubalozi wa Uswisi, yakiwa na dhamira ya kukuza ujuzi na ajira kwa vijana.