Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban amewataka vijana kushiriki michezo kwani michezo ni nyenzo muhimu katika kujenga afya, kutoa ajira kwa vijana na kutangaza amani katika jamii.
Akizungumza Julai 09, 2025 mbele ya mamia ya wakazi wa Kata ya Mlowo waliokusanyika kushuhudia tukio la uzinduzi wa Kombe la Polisi Jamii lililofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi Mlowo, Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.
ACP Akama alisema kuwa “Michezo si burudani pekee bali ni sehemu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwani Michezo ni njia ya kuwajenga vijana kimwili na kiakili, lakini pia inatoa ajira kwa maelfu ya watu, kuanzia kwa wachezaji, makocha, waamuzi hadi waandaaji wa matamasha na mashindano”
Aidha, Kamanda Akama aliwapongeza wananchi wa Mlowo kwa kuunga mkono juhudi za Jeshi la Polisi kupitia mashindano hayo, akieleza kuwa mashindano ya Polisi Jamii ni sehemu ya mkakati wa kuimarisha uhusiano kati ya Polisi na wananchi katika kupunguza uhalifu ikiwa ni pamoja na vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na kutokufanya unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto. Pia kupitia michezo inafanya tuwasiliana na kujifunza kushirikiana na tunajenga amani ya kudumu katika nchi yetu.
Uzinduzi huo uliambatana na mechi ya ufunguzi kati ya timu ya Forest FC na timu ya Changalawe FC ambayo Forest FC iliibuka kidedea kwa ushindi wa goli 01 dhidi ya Changalawe FC na kuchukua ngao ya Polisi Jamii ikiwa ni pamoja na kiasi cha pesa tasilimu kwa kitendo hicho jamii inaendelea kuhamasishwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe ikiwa ni pamoja na kupata elimu juu ya masuala ya ulinzi na usalama katika maeneo yao ili jamii iendelee kuwa salama.
Sambamba na hayo, ACP Akama alitoa wito kwa wazazi na walezi kuwahimiza watoto kushiriki katika michezo kama njia ya kuwajenga kiafya na kuwaepusha na vitendo vya kihalifu, tuwekeze kwenye michezo, tupate afya bora, amani na kukuza uchumi wa taifa letu ikiwa ni pamoja kuwachagua viongozi bora na sio bora viongozi katika kipindi cha uchaguzi wa mwaka 2025 kwa manufaa ya maendeleo ya taifa letu.
Naye, Mratibu wa Mashindano hayo, Mrakibu wa Polisi (SP) John Maro alisema dhumuni la mashindano hayo ni kuwaweka vijana na jamii pamoja ili kupunguza uhalifu katika kata ya Mlowo, huku akiongeza kuwa mashindano hayo yanatarajiwa kuendelea kwa wiki kadhaa yakihusisha timu kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Vwawa na Mlowo, huku yakilenga pia kutoa elimu juu ya masuala ya usalama kwa jamii.