Mageuzi makubwa yaliyofanyika katika sekta ya elimu nchini, hususan mafunzo ya Amali yameanza kuvutia mataifa mengine barani Afrika kuja kujifunza namna yalivyofanyika na utekelezaji wake.
Hayo yamebainishwa Julai 05, 2025 jijini Dodoma kufuatia ziara ya Waziri wa Elimu ya Juu, Utafiti, Sayansi na Teknolojia kutoka Jamhuri ya Gambia Prof. Pierre Gomez ambaye amesema lengo la kufika Tanzania ni kujifunza mbinu zilizotumika katika kufanya maboresho na maugezi makubwa katika sekta ya elimu.
Waziri huyo amesema kuwa Benki ya Dunia iliishauri nchi hiyo kuja Tanzania ili kujionea namna utekelezaji wa Sera, mikakati na miradi mbalimbali katika sekta ya elimu ili kuwawezesha kutekeleza miradi yao kwa ufanisi na tija.
“Tumeshuhudia ujenzi wa miundombinu na mifumo ya mafunzo ya vitendo yenye tija katika vyuo mbalimbali ikiwemo DIT, VETA na Taasisi, tunaamini kunufaika zaidi kupitia ushikiano katika nyanja mbalimbali za mafunzo” Alisema Prof. Gomez.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa Tanzania Prof. Adolf Mkenda amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na Gambia katika kubadilishana wakufunzi na wanafunzi ili kuimarisha uhusiano wa kielimu kati ya nchi hizo mbili.
“Tunaamini kuwa kwa kushirikiana, tutaweza kuinua viwango vya elimu ya amali barani Afrika na kusaidia vijana kupata ujuzi unaohitajika katika soko la ajira,” alisema Prof. Mkenda.
Ziara hii ni ushahidi wa namna mageuzi ya elimu nchini yanavyotambuliwa kimataifa, na jinsi ambavyo nchi inavyojenga nafasi yake kama kitovu cha ubunifu na ubora katika elimu ya amali Afrika.