Katibu tawala mkoa wa Katavi Albert Msovela akizungumzia na wanahabari.
Na. Mwandishi wetu, Katavi.
Mkoa wa Katavi umeandaa tamasha la siku mbili kwa lengo la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari katibu tawala wa mkoa wa Katavi Albert Msovela amesema mkoa wa Katavi ulipokea kiasi cha shilingi trilioni 1.345.
Bwana Msovela amesema tamasha hilo litafanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 4 hadi 5 Julai mwaka huu.
Ameeleza kuwa katika siku ya kwanza ya tamasha hilo timu ya Kizimkazi, viongozi na wataalam mbalimbali watafanya utalii katika Hifadhi ya Katavi, pamoja na kutembelea miradi katika manispaa ya Mpanda.
Pamoja na miradi itakayotembelewa ni mradi mkubwa wa maji wa miji 28, vihenge vya mazao (NFRA), hospitali ya rufaa ya mkoa na kituo cha kupoozea umeme wa gridi ya Taifa.
Aidha katika siku ya pili ya tamasha hilo itakayofanyika Inyonga wilayani Mlele kutakuwa na matembezi ya hiari, michezo mbalimbali na kupokea taarifa ya miradi mbalimbali iliyofanyika.
Katibu tawala huyo wa mkoa wa Katavi ametoa rai kwa makundi mbalimbali ya wananchi kujitokeza katika tamasha hilo.
Ametaja kauli mbiu ya tamasha hilo kuwa ni “Asante rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha za maendeleo, Katavi imara na maendeleo imara”.