NA DENIS MLOWE IRINGA
WATAALMU wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wametoa elimu kwa umma kuhusu mikopo salama pamoja na utaratibu wa kupata leseni ya utoaji wa huduma za kifedha ikiwalenga wafanyabiashara, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza na wanahabari katika mahojiano maalum, Afisa Sheria Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) , Ramadhani Myonga alisema kuwa
Mampeni hiyo ya kutoa elimu inatekelezwa kufuatia matokeo ya uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na BoT kupitia ripoti maalumu iitwayo Kimangala Report, ambayo ilibaini kuwa wakazi wa mkoa wa Iringa ni miongoni mwa waathirika wa mikopo isiyo rafiki inayojulikana kama “mikopo umiza” au Kimangala.
Alisema kuwa elimu hiyo inatolewa ili kuwaelimisha wananchi kwa ujumla juu ya kubaini mikopo salama kutoka katika taasisi mbalimbali za kifedha zilizosajiliwa na benki kuu ya Tanzania.
Myonga ammewaasa wananchi pindi wanapotaka kuchukua mkopo kutoka kwenye Taasisi za Kifedha basi ni muhimu wajue mambo mbalimbali juu ya Taasisi husika wanazotaka kukopa ziwe na leseni halali kwani itasaidia pale ambapo utapata tatizo katika mkopo wako kuwachukulia hatua za kisheria, kwani Taasisi ikikosea masharti iliyopewa na Benki Kuu huweza kufutiwa Leseni na kufungiwa huduma.
Aliongeza kuwa pamoja kila Taasisi ya Fedha lazima iwe na dawati la kutatua migogoro kati yao na mteja, na kwamba mgogoro unapowasilishwa katika dawati hilo, ni lazima utatuliwe ndani ya siku 14, kama utakuwa bado basi huongezwa siku saba ikishindikana hapo mteja anaweza kuwaandikia Benki Kuu na kuwasilisha mgogoro wake na Taasisi husika.
Alisisitiza kuwa wananchi wanatakiwa kabla ya kwenda kukopa wawe makini zaidi kwa kusoma mkataba wa ukopeshaji ni muhimu sana kabla ya kusaini mkataba huo aelewe vipengele vyake na kuacha kukimbilia kusaini.
Myonga vile vile alisema wakopaji wanatakiwa kuzingatia lengo la mkopo unaokopa usikope kwa ajili ya shughuli isiyokuwa na maendeleo wengine wanakopa wanaenda fanyia sherehe hii kusababisha wengi kushindwa kurudisha mkopo.
“Ukiwa na mkopaji rejesha kwa wakati kwani mkopo sio sadaka na hakikisha unatunza kumbukumbu zako za mrejesho wa fedha zako na kuweka nyaraka muhimu za mkopo ambao ni mkataba uliosaini ili kukusaidia pindi ukipata changamoto ‘”alisema
Vile vile alisema kuwa haki na wajibu wa mkopaji kuhakikisha sehemu anayokopa ina leseni na taasisi ya fedha kumpa elimu anayetaka kukopa kabla ya kumpa mkopo na kuongeza kuwa wajibu wa mkopaji ni kulipa kwa wakati deni kwani usiporejesha utaingia changamoto ambayo itaeleta utata na mkopeshaji.
Kwa upande wake Mchungaji Ombeni Sawike ambaye ni mmoja wa Walimishaji waliopewa mafunzo na benki kuu ya Tanzania aliwashukuru BOT kwa kutoa mafunzo kwani yamemfanya kuelewa elimu ya uwekezaji katika mifuko mbalimbali hali ambayo hapo awali hakujua.
Alisema kuwa watu wengi wamekuwa wakikopa mikopo bila kuzingatia mikataba wanayoingia katika kukopa hivyo hutoa elimu kwa watu mbalimbali juu ya mikopo baada ya kupata mafunzo hayo.
Aliwaasa wananchi kuwa makini katika mikopo wanayokopa ili wasiingie katika mikopo umiza ambayo haizingatii Sheria za nchi.



