MKUU wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA mafanikio ambayo hayajawahi kushuhudiwa kabla, Mkoa wa Kagera umeingia katika historia kwa vijiji vyake vyote 662 kuunganishwa na umeme kwa mara ya kwanza, hatua inayotajwa kuongeza tija kwenye sekta za kilimo, elimu, afya na biashara.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Julai 1,2025 jijini Dodoma kuhusu Mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi April 2025 .
Mhe.Mwassa amesema mafanikio hayo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya Serikali ya Awamu ya Sita, ambapo zaidi ya Shilingi trilioni 1.131 zimetumika katika kipindi cha Novemba 2020 hadi Aprili 2025 kuleta mageuzi ya kijamii na kiuchumi.
“Kwa mara ya kwanza katika historia ya mkoa huu, kila kijiji kimepata umeme. Hii ni hatua kubwa ya kuamsha uchumi wa kaya, kuongeza usalama na kuboresha huduma muhimu,” alisema Mwassa.
Amesema mbali na mafanikio kwenye sekta ya nishati, huduma za afya zimeimarika kwa kiwango kikubwa, ambapo hospitali zimeongezeka kutoka 3 hadi 11, vituo vya afya kutoka 29 hadi 42, na zahanati kutoka 217 hadi 283, huku wagonjwa waliotibiwa ndani ya mkoa wakiongezeka kwa asilimia 273 kutokana na upatikanaji wa huduma za kibingwa na vifaa tiba vya kisasa.
Kwa upande wa elimu, ameeleza kuwa Serikali imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 128, kujenga shule mpya 116 za msingi na awali, sekondari 68, vyuo vya VETA kutoka 4 hadi 9, na kuongeza ufaulu wa sekondari kutoka asilimia 91 hadi 94.57.
Sekta ya maji nayo imepata msukumo mpya baada ya kutekelezwa kwa miradi 41 yenye thamani ya Shilingi bilioni 164.7, ambapo huduma ya maji safi mijini imeongezeka hadi asilimia 93 na vijijini hadi asilimia 83.
Katika miundombinu, barabara na madaraja yameboreshwa kwa Shilingi bilioni 117.9, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Kitengule na barabara ya Bugene–Kasulo–Kumunazi. Idadi ya madaraja imefikia 468, na barabara za mijini zimeongezeka hadi km 40.87.
Mkoa wa Kagera ambao unakadiriwa kuwa na wakazi zaidi ya milioni 2.9 kwa mujibu wa Sensa ya 2022, pia umepiga hatua kwenye kilimo, hasa cha kahawa, baada ya Serikali kupunguza tozo kutoka 17 hadi 5. Hatua hiyo imechochea kupanda kwa bei kutoka Shilingi 1,200 hadi 4,200 kwa kilo na kuongeza uzalishaji hadi tani 54,203 kwa mwaka.
Ameongeza kuwa wananchi wamewezeshwa kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kutoka Shilingi bilioni 3.2 hadi bilioni 9.4, huku kaya maskini 380,035 zikifaidika na mpango wa TASAF.
Idadi ya biashara rasmi mkoani Kagera imeongezeka kwa asilimia 55, na wawekezaji waliosajiliwa kupitia TIC wamefikia 275 waliowekeza miradi ya zaidi ya Shilingi bilioni 267.1, na kutoa ajira kwa watu zaidi ya 11,000.
Kwa mujibu wa Mwassa, mapato ya ndani ya halmashauri za mkoa huo yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 23.6 mwaka 2020/21 hadi bilioni 47.2 mwaka 2024/25, huku mkoa ukitekeleza miradi 28 ya kimkakati kwa kutumia fedha hizo, ikiwemo masoko, shule za michepuo ya Kiingereza, stendi za mabasi na barabara mpya ndani ya Bukoba.
“Mkoa wa Kagera umedhihirisha kuwa sera na mipango ya Serikali ya Awamu ya Sita inaweza kuleta matokeo ya haraka na ya kuonekana, endapo kutakuwa na usimamizi thabiti na ushirikiano wa wananchi,” alisema Mwassa.