Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za kisheria kwa umma kutoka wizara ya Katiba na Sheria Bw.Abdulrahman Msham, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Banda la Wizara hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika Leo Juni 23,2025 katika Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna_DODOMA
WANANCHI 231 wamepatiwa msaada wa Kisheria Katika maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika Jijini Dodoma kuanzia Juni 16 Hadi 23, 2025.
Hayo yameelezwa Leo Juni 23,2025 na Mkurugenzi Msaidizi wa huduma za kisheria kwa umma kutoka wizara ya Katiba na Sheria Bw.Abdulrahman Msham wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Banda la Wizara hiyo wakati wa kilele cha maadhimisho hayo.
Msham amesema kuwa wizara hiyo imetumia maadhimisho hayo Kwa kutoa huduma za msaada wa kisheria kwa jamii.
Aidha amesema idadi kubwa ya wananchi waliyofika katika banda hilo walikuwa na changamoto za migogoro ya Ardhi,mirathi na migogoro ya ndoa ambapo ameahidi kuwa wizara ya katiba na sheria itahakikisha inaitatua migogoro hiyo ili wananchi waishi kwa usalama.
“Wizara ya katiba na sheria ni miongoni mwa wizara 23 zilizo shiriki maadhimisho haya tangu yalipo anza tarehe 16 mwezi wa sita hadi leo tarehe 23,wizara yetu inayo majukumu makubwa matatu ikiwa na dhamana ya kusimamia sheria zote na mfumo wa haki nchini.
“Kama wizara ushiriki wetu hapa pamoja na kuonesha nini wizara inakifanya lakini imeendelea kutoa huduma zake kwa wananchi ambao wametembelea banda letu na tangu tuanze hadi leo jumla ya wananchi 231 wame hudumiwa katika banda hili wakipatiwa huduma ya ushauri wa kisheria,” amesema.
Aidha amesema wizara hiyo haipo nyuma na mabadiliko ya ukuaji wa teknolojia ambapo imeendelea kutoa huduma zake kupitia mfumo wa kidijitali ukiwemo mfumo wa kusajili utetezi wa migogoro kwa njia mbadala pamoja na mfumo wa kusajili wasaidizi wa sheria.
Hata hivyo amesema wizara hiyo imejipanga kuendelea kutoa huduma za ushauri na msaada wa kisheria katika maonesho mbalimbali yakiwemo maonesho ya sabasaba na nanenane mwaka huu.