Wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu wameonesha mwitikio mkubwa katika kushiriki zabuni za serikali kupitia mfumo wa kielektroniki wa usajili wa ununuzi wa umma (NeST).
Haya ni matokeo ya jitihada zinazofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuhakikisha makundi maalum yanashirikishwa kikamilifu katika fursa za kiuchumi nchini.
Akizungumza katika mafunzo maalum yaliyofanyika jijini Dodoma kwa wanawake kutoka mikoa ya Singida, Dodoma, Arusha na Kigoma, Afisa wa PPRA Bw. Wilson Samweli ameeleza kuwa mwitikio wa wanawake katika kushiriki mchakato wa zabuni kupitia mfumo wa NeST ni mkubwa na wa kutia moyo.
“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo wanawake kushiriki kikamilifu katika zabuni za serikali. Mfumo wa NeST unawawezesha kujiandikisha na kushiriki kwa uwazi na usawa,” amesema Bw. Samweli.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa uwezeshaji wanawake kiuchumi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya usawa wa kijinsia (UN Women), Michael Jerry amesema mafunzo hayo ni fursa ya kipekee kwa wanawake kuwa sehemu ya mnyororo wa manunuzi ya umma.
“Mafunzo haya yatasaidia wanawake kujua namna ya kuandaa nyaraka za zabuni, kutumia mfumo wa NeST na hivyo kupata nafasi zaidi katika kushindania tenda za serikali,” ameeleza Jerry.
Afisa biashara kutoka Mkoa wa Kigoma, Baraka Meleck amebainisha kuwa ushiriki wa wanawake katika zabuni za serikali unaongeza maendeleo ya jamii kwa kuwa mwanamke akinufaika kiuchumi, familia na jamii nzima hunufaika.
Ester Salanga, mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, amesema kuwa mafunzo waliyopata yamewawezesha kuelewa taratibu za kushiriki zabuni, jambo ambalo limesaidia kuboresha biashara zao na kuongeza kipato.
“Awali tulikuwa hatujui namna ya kushiriki zabuni za serikali, lakini sasa tunajua hatua zote na tunapambana kuingia kwenye ushindani,” amesema Ester kwa furaha.
PPRA inaendekea kutoa mafunzo kama haya katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza ushiriki wa makundi maalum katika uchumi wa taifa.