Mhifadhi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru akionesha pango lililotumika na mashujaa wa wamatengo kuhifadhi miili ya watu 400 kwa wakati mmoja lililopo eneo la Litembo wilayani Mbinga
Mhifadhi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbinga Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru akielezea namna wajerumami walivyowauwa kikatili mashujaa 800 wa kabila la wamatengo mwaka 1902 katika kijiji cha Litembo wilayani Mbinga
MNARA wa makunbusho ya mashujaa wa majimaji uliojengwa eneo ambalo waliuawa mashujaa 800 na wajerumani mwaka 1902
ENEO la kaburi la pamoja ambalo watu 800 walizikwa baada ya kuuawa na wajerumani mwaka 1902,eneo hili linatakiwa kuboresha kwa kujengwa vuzuri ili kuwaenzi mashujaa hao
Na Albano Midelo
Jua lilipozama Machi 4, 1902, milima ya Umatengo haikulisindikiza kwa machweo ya kawaida.
Badala yake, anga lilitawaliwa na moshi mzito wa bunduki, vilio vya kina mama, na sauti za mwisho za mashujaa waliokataa kupigishwa magoti na mkoloni wa Kijerumani.
Ni siku ambayo historia ya Tanzania ilichorwa kwa damu na si damu ya kawaida, bali ya mashujaa wapatao 800, waliolala milele katika ardhi ya Litembo wilayani Mbinga mkoani Ruvuma kwa ajili ya kulinda heshima, ardhi, na uhuru wa kizazi cha leo.
Litembo: Jiwe Lililobeba Ujasiri
Katika kijiji kidogo cha Litembo,lipo jiwe kubwa linalofanana na kichwa cha tembo. Jiwe hilo si tu kivutio cha kijiografia, bali ni nembo ya ushujaa wa Wamatengo.
Chini yake kuna pango refu lenye njia mbili moja ya kuingia, nyingine ya kutokea. Hapo ndipo mababu wa kabila la Wamatengo walijificha na kujipanga dhidi ya jeshi la wakoloni wa Kijerumani waliokuja wakibeba bunduki 19 na dhamira ya kutwaa ardhi kwa nguvu.
Mhifadhi na Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mbinga, Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru, anakumbuka historia hiyo kwa uchungu:
“Walituambia tushushe bendera yetu. Wakadai nchi hii sasa iko chini ya himaya ya Mjerumani. Wazee wetu walikataa. Hilo halikukubalika. Walijipanga, wakaingia mapangoni, wengine wakabaki nje kupambana. Wakoloni wakaanza kulimiminia risasi jiwe la Litembo. Watu wetu walipigwa risasi hadi kufa zaidi ya mia nane.”
Jiwe Lililotoa Damu, Mto Uliojaa Machungu
Picha ya maangamizi ilikuwa ya kusikitisha. Mto Litembo, uliokuwa chemchemi ya uhai kwa vijiji vya jirani, uligeuka kuwa mto wa damu.
Risasi za Wajerumani zilichuruzika kwenye ngozi za mashujaa wasio na silaha za kisasa. Walijibu kwa mishale, mikuki, na moyo wa ushujaa wa hali ya juu. Lakini hawakuweza kushindana na risasi za moto.
Katika machafuko hayo, mashujaa waliouawa walizikwa kwenye makaburi ya pamoja, yaliyopewa jina la Hola Hola. Salvius Simon Komba, Mwenyekiti wa Mila kata ya Litembo, anasimulia:
“Lile pango lilitumika kuhifadhi miili. Linaweza kuchukua watu 400 kwa wakati mmoja. Lakini idadi ya waliokufa ilizidi uwezo wake. Hata leo, ukichimba ardhini eneo hili, utakuta masalia ya miili mifupa, vichwa, hadi mabaki ya silaha za jadi.”
Ukatili wa wakoloni haukuishia kwenye bunduki
Ukatili wa wakoloni haukuishia tu kwa risasi. Waliamua kuchoma maghala ya chakula, kuteketeza nyumba, na kuacha jamii nzima ya Wamatengo ikikumbwa na njaa kali.
Bruno Tembo, Katibu wa Baraza la Mila kata ya Litembo, anakumbusha kuwa, kiongozi wa Wajerumani aliyejulikana kama Korongo, ndiye aliyetoa amri ya shambulio hilo baada ya Chifu Kawania wa Wamatengo kukataa kushirikiana naye.
“Baada ya mashujaa wetu kukataa kutawaliwa, Korongo alileta askari na silaha. Lakini mababu zetu walijipanga. Walijificha kwenye pango, wengine walikaa nyuma ya jiwe. Vita ikaanza. Lakini walizidiwa na risasi.”
Mnara wa Kumbukumbu: Alama ya Mashujaa Waliosahaulika
Mnamo mwaka 2004,Mbunge Mstaafu Mheshimiwa Ngwatura Ndunguru alisimamia ujenzi wa mnara wa kumbukumbu katika eneo la jiwe la Litembo.
Mnara huo, uliowekwa maandishi ya sonara, ni alama ya heshima kwa waliolala milele kwa ajili ya kizazi hiki.
“Maandishi yameanza kufifia, lakini ujumbe wake bado unaishi. Mnara huu unahitaji ukarabati na eneo hili lina kila sifa kuwa Makumbusho ya Kitaifa, lakini bado halijatambuliwa rasmi. Ni wakati sasa Serikali ichukue hatua,” anasisitiza Ndunguru.
Litembo si tu historia ya Mbinga. Ni historia ya Taifa. Ni mfano hai wa mapambano ya kiafrika dhidi ya ukoloni. Ni eneo linalopaswa kuwa darasa la historia, kivutio cha utalii wa kihistoria, na kitovu cha uzalendo wa kizazi kipya.
Salvius Nyamajabeni, Mwenyekiti wa Baraza la Mila tangu 1958, anatoa rai nzito:
“Hatuwezi kuendelea kuwasahau mashujaa waliotufia. Serikali iwekeze hapa. Tuoneshe kizazi kipya kwamba uhuru hauna thamani kama hatukumbuki damu iliyomwagika kuupata.”
Litembo ni zaidi ya jiwe. Ni kaburi la mashujaa 800, darasa la kizazi, na ukumbusho wa bei ya uhuru. Tunapokimbizana na maendeleo ya kisasa, tusisahau walikodondoka mashujaa wetu.
Tusipojenga makumbusho yao, basi tuwe tayari kuona historia ikipotea.