Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe, amewaagiza Watendaji wa Wizara ya Kilimo kuhakikisha mchakato wa ununuzi wa ndege mpya tatu unaanza kwa ajili ya vituo vya Kilimo Anga vya kanda vilivyopo katika mikoa ya Arusha,Mbeya na Mwanza ili kusaidia katika udhibiti wa visumbufu vya mimea.
Waziri Bashe ametoa rai hiyo Mei 30,2025 jijini hapa Dodoma wakati wa hafla ya mapokezi ya ndege moja ya kudhibiti visumbufu vya mimea iliyonunuliwa na Serikali nchini kupitia Wizara hiyo ambayo itatumika katika kituo cha Kanda ya Kati.
“Leo tumeweka histori katika Taifa letu na hii ni kwa mara ya kwanza Tanzania inanunua ndege yake yenyewe itakayo saidia katika kilimo cha anga na siku zote tumekuwa tukikodisha ndege kutoka nchi nyingine ikiwo Kenya,”amesema.
Aidha, Waziri Bashe amesema Tanzania ni mara na ya kwanza kumiliki aina hiyo ya ndege, licha ya kuwa uhitaji wake umekuwepo kila wakati na serikali imekuwa ikikodisha ndege kutoka nje ya nchi kwaaji ya shughuli za upuliziaji dawa kwa wadudu na ndege ambao wamekuwa wakivamia mashamba na kuharibu mazao ya wakulima.
“Sasa tumeanza na ndege moja ila lengo lrletu tuwe nazo kama nne na Vituo vyote hivi vinatakiwa viwe vina ndege na ‘drones’ kwa hiyo, mchakato wa kununua ndege tatu nyingine uanze sasa hivi. Ni lazima kama Nchi ijitegemee, dunia ya kubebana haipo. Lazima tuweze kutoa huduma, tumeshaanza kununua ‘drones’ za kufanya ‘survilence’, mwaka huu tunanunua drone kwa ajili ya ‘spraying,”amesema Waziri Bashe.
Katika hatua nyingine Mhe.Bashe amewahimiza wakulima kote nchi kujikita hasa katika kilimo cha umwagiliaji kutokana na kuzinduliwa kwa ilani ya chama cha mapinduzi CCM itakayo nadiwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kuwa ilani hiyo zaidi ya asilimia 70% imezungumzia sekta ya kilimo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) Prof. Joseph Ndunguru, amesema ndege hiyo inalenga kuleta mageuzi makubwa katika Sekta ya Kilimo kwa kuleta tija, ajira na kupanua masoko pamoja na kuimarisha hali ya chakula hapa nchini .
Aidha amesema kuwa ndege hiyo aina ya ‘Thrush 510 P2’ imenunuliwa kwa gharama ya TSh.Bilioni 6 huku akisema kuwa ina uwezo wa kukaa angani kwa zaidi ya masaa manne kutokana na tenki lake kubeba mafuta yenye ujazo wa lita 863 na ikiwa na uwezo wa kubeba viuatilifu lita 1,930 uwezo wa kufanya udhibiti kwenye eneo la ekari 2400 kwa mara moja huku ikiwa na vifaa vya kisasa kwa ajili ya kutolea takwimu zinazowezesha mpango wa uthibiti wadudu na ndege waharibifu wa mazao na mimea.
“Ndege hii imenunuliwa kwa shilingi Bilioni 6 chini ya serikali ya awamu ya sita na hizi ni juhudi za mhe.rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini,”amesema.