Naibu Waziri wa Fedha Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), akijibu swali la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichalwe, alietaka kujua mpango wa dharura wa Serikali wa kudhibiti utoroshaji wa bidhaa nje ya nchi kwa njia za magendo na Serikali itaanza lini ujenzi wa Kituo cha Forodha Momba ili kupunguza Msongamano wa Magari Tunduma Mkoani Songwe, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)
Peter Haule, WF, Dodoma
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb) ametoa agizo kwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha anaimarisha doria kwenye mipaka hususani maeneo yanayotumika kupitisha bidhaa kwa njia ya magendo Wilayani Momba mkoani Songwe kwa kushirikiana na wadau wengine.
Agizo hilo amelitoa bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Momba, Mhe. Condester Michael Sichalwe, aliyetaka kujua mpango wa dharura wa Serikali wa kudhibiti utoroshaji wa bidhaa nje ya nchi kwa njia za magendo.
Aidha, akijibu swali la msingi la mbunge huyo kuhusu lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Forodha Momba ili kupunguza Msongamano wa Magari Tunduma Mkoani Songwe, Mhe. Chande alisema kuwa Serikali inafanya Upembuzi yakinifu ili kupata taarifa muhimu kwa kuanzishwa kwa kituo cha forodha Wilaya ya Momba
Alisema kuwa upembuzi yakinifu unafanywa katika mwaka huu wa fedha 2025/26, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na idara mbalimbali za Serikali zinazohusika na shughuli za kiforodha mipakani.