Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari kwenye wiki ya Nordiki 2025 Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KATIBU Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi za Nordiki ambzo ni Denmark, Finland, Norway na Sweden katika kuangalia fursa zilizopo katika uzalishaji wa nishati jadidifu.
Mhandisi Mramba ameyasema hayo leo Mei 26,2025 jijini Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Nordiki 2025 inayofanyika kuanzia leo Mei 26 hadi 29, 2025 ikiwa inaadhmishwa katika Mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro.
“Lakini pia tunaangalia katika maeneo mengine ya kiufundi ambayo wanaweza kuisaidia Tanzania na makampuni ya ndani yakaweza kushirikiana na mataifa hayo katika kuwezesha utekelezaji wa mpango huo,”amesema.
Aidha, amesema eneo lingine ni uwekezaji katika miradi ya uunganishaji wa umeme katika nchi moja kwenda nchi nyingine ambapo kwasasa Tanzania inataka kuunganisha na nchi jirani zake pamoja na ndani ya nchi.
Amesema tangu uhuru mataifa hayo yamekuwa yakishirikiana na Tanzania kwenye eneo la nishati pamoja na kutoa mikopo katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza umeme nchini.
Wiki ya Nordiki ya mwaka huu inafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Mabadiliko ya Kijani na Kidijitali kwa Mustakabali Endelevu”, ikilenga kushughulikia changamoto za kimataifa kama vile mabadiliko ya tabianchi na mageuzi ya kiuchumi kupitia mkusanyiko wa makongamano, warsha, maonyesho, burudani za kitamaduni na matukio shirikishi kwa umma.
Lengo kuu la wiki hiyo ni kukuza taswira ya kisasa, jumuishi na ya vitendo ya nchi za Nordiki pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Nordiki na Tanzania.
Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania ,Tone Tinnes,amesema kuwa nchi za Nordiki zitaendelea kuhakikisha zinawekeza zaidi katika Nishati Jadidifu,ikiwa ni njia muhimu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi


Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Mhandisi Felchesmi Mramba akizungumza na waandishi wa habari kwenye wiki ya Nordiki 2025 Jijini Dodoma.

Balozi wa Norway nchini Tanzania Tone Tinnes akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Nordiki 2025 Jijini Dodoma.








