Umoja wa Washiriki wa Mapenzi ya Jinsia Moja nchini Tanzania, umeungana na Bunge la Umoja wa Ulaya kutaka kuachiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, bila masharti yoyote.

Wakizungumza kupitia msemaji wao ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu za kiusalama, wamesema kuwa kesi inayomkabili Lissu ni ya kupangwa kutokana na msimamo wake wa kutetea haki za binadamu bila ubaguzi.

“Tunaunga mkono kauli ya No Reforms, No Election kwa sababu mabadiliko ya kisiasa na kisheria yatawezesha kulindwa kwa haki za watu wote,” amesema msemaji huyo.

Umoja huo umetoa wito kwa Serikali na jamii kwa ujumla kutambua uwepo wao kama sehemu ya jamii ya Watanzania, na kudai kuheshimiwa sawa na makundi mengine.

Aidha, wamewataka viongozi wa dini kuacha kuwatenga na kutumia dini kama chombo cha kuwakandamiza, huku wakisisitiza kuwa kila mtu ana haki ya kuabudu dini aipendayo mradi havunji sheria za nchi.

“Tunazisihi taasisi mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia na vyama vya siasa kupaza sauti kuunga mkono haki zetu kama tunavyoheshimu haki za jamii nyingine,” amesema msemaji huyo.

Umoja huo umeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ndani na nje ya nchi katika kutetea na kuelimisha jamii kuhusu haki sawa kwa wote.