Na Mwandishi wetu
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, dk Selemani Jafo, ameagiza kuanzishwa kwa oparesheni maalumu ya kuwabaini na kuwaondoa wageni wanaofanya biashara kinyume cha sheria katika Soko la Kariakoo mkoani Dar es Salaam.
Dk Jafo ametoa agizo hilo leo Mei 5,2025 alipotembelea soko hilo na kufanya mazungumzo na baadhi ya wafanyabiashara, ambapo alieleza kusikitishwa na kile alichokiita “uvamizi wa kibiashara” unaofanywa na baadhi ya wageni wanaofanya biashara zilizotengwa kwa ajili ya wazawa.
“Nimejiridhisha kuwa kuna idadi kubwa ya wageni wanaofanya biashara za wazawa kwa kutumia majina ya Watanzania, hali inayowanyima fursa wazawa wetu na kuchochea ushindani usio wa haki,” amesema dk Jafo.
Amesema oparesheni hiyo itashirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na taasisi zote zinazohusika na biashara, na itahakikisha sheria za biashara zinafuatwa kikamilifu.
“Nawaagiza viongozi wa mkoa na taasisi husika kuchukua hatua haraka. Hii ni vita ya kulinda uchumi wa Mtanzania mnyonge,” alisisitiza waziri huyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema changamoto ya wageni kufanya biashara kwa kutumia majina ya wazawa imechangia ongezeko la gharama za upangaji wa maduka sokoni hapo.
“Wageni hawa wanapanga maduka kwa bei ya juu, hali inayowafanya wafanyabiashara wetu kushindwa kumudu gharama hizo,” amesema Mpogolo.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Hamis Luvembe ameunga mkono hatua ya serikali, akisema kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa, uchumi wa wafanyabiashara wazawa utaporomoka.
“Wageni hawa wanapora mitaji ya watanzania. ushindani ni sawa, lakini si kwa njia ya ujanja ujanja wa kutumia majina ya wazawa,” amesema
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Severin Mushi, amesema wafanyabiashara wamefarijika na hatua ya serikali na wana matumaini kuwa oparesheni hiyo itasaidia kurejesha hali ya amani na haki sokoni.
“Tuna imani kubwa kwa waziri ametusikiliza na sasa tunasubiri utekelezaji wa haraka ili kuokoa biashara zetu,” amesema Mushi.
Ziara ya dk Jafo imekuja wakati ambapo kumekuwepo na malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu ushindani usio wa haki kutoka kwa wageni wasio na vibali halali vya kufanya biashara nchini.
Serikali imeeleza dhamira yake ya kuhakikisha kuwa mazingira ya biashara nchini yanabaki kuwa ya haki, salama na yenye ushindani wa kweli kwa watanzania.