*Naibu Waziri Mawasiliano aipongeza kwa kuwafikia Wananchi wa vijijini*
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaendelea zoezi la kuhamasisha na kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambapo Wananchi wa kijiji cha jojo, kata ya Santilya, tarafa ya Isangati, Halmashauri ya Mbeya vijijini, wamefikiwa na huduma hiyo kupitia maonesho maalum yaliyopewa jina la Wakulima Festival.
Akifungua maonesho hayo, tarehe 27 Aprili, 2025, Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Maryprisca Mahundi amepongeza juhudu zinazofanywa na Wakala wa Nishati Vjijini (REA) katika kuwafikia Wananchi wa vijijini hususan katika kuhamasisha na kuelimisha kuhusu matumizi ya teknolojia za nishati safi ya kupikia katika kulinda afya za Watu, kulinda na kutunza mzingira pamoja na kusambaza teknolojia hizo.
“Naipongeza REA kwa kufika hapa kata ya Santilya, kijiji cha Jojo, ili kuhamasisha na kuelimisha Wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, mmetoka mijini na mmekuja vijijini”…
“Matumizi ya nishati safi, ni kampeni maalum ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kumpunguzia Mwanamke mzigo mkubwa wa kupika kwa kuni pamoja na athari za kiafya na kimazingira ili pia ashiriki kwenye shughuli nyengine za maendeleo”. Alisema Naibu Waziri, Mhandisi, Maryprisca Mahundi.
Awali, akimkaribisha kwenye banda la REA, Mhandisi Miradi ya Nishati Safi kutoka REA, Raya Majallah alisema, REA imeendelea kutekeleza Miradi ya kusambaza nishati mbalimbali vijijini na baada ya kutekeleza jukumu la kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vya Tanzania Bara, sasa msukumo umewekwa kwenye kusambaza umeme kwenye vitongoji pamoja na kusambazaji wa Miradi ya nishati safi ya kupikia, ambapo Mradi wa kusambaza majiko banifu, mitungi ya gesi na majiko yake pamoja na kutoa mikopo mafuu ya ujenzi wa vituo vidogo vya kusambaza bidhaa za mafuta ya petrol na dizeli inaendelea kutekelezwa kikamilifu.
“REA kwa kushirikiana na Wadau (Sekta Binafsi) tumefika hapa kijiji cha Jojo ili kuelimisha na kuhamashisha matumizi ya nishati safi, na kwa kuwa umeme upo kijijini, tunahamasisha matumizi ya majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo (Yanayotumia uniti 1 kwa saa) pamoja na majiko banifu yanayotumia mkaa au kuni kidogo”. Amesema, Mhandisi, Raya Majallah.