NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa ngazi za Matawi,Wadi,Majimbo ya CCM Wilaya ya Micheweni katika mwendelezo wa ziara ya ya kuimarisha uhai wa Chama na Jumuiya zake katika ziara yake ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar huko Micheweni Kisiwani Pemba leo tarehe 28/04/2025.
NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,ameziagiza Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Wizara ya Maji,Nishati na Madini Zanzibar kumaliza changamoto za malalamiko ya Wananchi juu ya urasimu wa kuungiwa huduma ya umeme pamoja na huduma duni za Afya katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni.
Ametoa wiki moja kuletewa ripoti ya utekelezaji wa maagizo hayo kwa Wizara husika ili wananchi wa Wilaya hiyo na maeneo mengine kisiwani Pemba waendelee kupata huduma bora na zenye viwango kama ilivyokusudiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema CCM ipo kwa ajili ya kusimamia Serikali itoe huduma bora kwa wananchi bila ubaguzi wa duni,rangi,kabila na itikadi za kisiasa na kwamba Chama hicho hakitovumilia viongozi na watendaji wasiotekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Hayo ameyasema katika mwendelezo wa ziara yake ya Sekretarieti ya Kamati maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar ya kuimarisha uhai wa Chama wakati akizungumza na wajumbe wa Kamati za siasa ngazi za matawi,wadi,majimbo na Wilaya ya Micheweni kichama katika ukumbi wa mikutano uliopo micheweni kisiwani Pemba.
Amesema wapo baadhi ya watendaji na viongozi Serikalini wamekuwa wakifanya urasimu wa kuchelewesha au kuwakosesha huduma muhimu wa wananchi kwa kusudi ili ionekane Serikali haitekelezi ahadi zake kwa wakati.
Dkt Dimwa,ameweka wazi kuwa kila ikikaribia wakati wa uchaguzi kuna baadhi ya watendaji wasiokuwa waadilifu wamekuwa hawafanyi kazi kwa ufanisi na kusababisha malalamiko yasiyo ya lazima.
“Kuna malalamiko mengi Pemba ya baadhi ya maeneo kukatika umeme mara kwa mara na wengine wakitaka kuungiwa umeme kuna urasimu pia zipo Hospitali zina vifaa tiba vya kisasa,zina madaktari wa kutosha dawa zote lakini bado wananchi hawapati huduma bora za Afya kwa wakati,,,naelekeza niletewe ripoti ndani ya wiki moja changamoto hizo ziwe zimemaliza.
CCM ndio tunaosimamia Serikali kuhakikisha inatekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025 kwa ufanisi,,,,hatucheki na mtu ukiona wewe ni mtendaji huwezi kufanya kazi serikalini acha kazi waajiriwe wengine”.
alisema Dkt Dimwa.
Katika maelezo yake Dkt.Dimwa,amesema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha uhai wa Chama na kuwakumbusha viongozi hao umuhimu wa kujiandaa na uchaguzi mkuu wa dola wa mwaka 2025.
Amewataka viongozi hao kuwahamasisha wanachama mbalimbali wenye nia ya kugombea kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu katika uchaguzi wa ndani wa kura za maoni ili wapate haki ya kidemokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa.
Alisema CCM itatenda haki na haitomuonea mtu yeyote hivyo kila mtu atapata haki yake kulingana na vigezo vya uteuzi vilivyowekwa na vikao vya juu.
Alitumia ziara hiyo kukemea vitendo vya rushwa,fitna na kuchagua na kisiasa na kwamba uchaguzi huo wa kura za maoni usiwagawe na kutengeneza migogoro ndani ya Chama badala yake uwaunganishe wanachama wote na kuunda umoja wenye nguvu za kupatikana ushindi katika uchaguzi wa dola wa Octoba 2025.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja Mjumbe wa Kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo Salama Mbarouk Khatib,alisema alieleza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa hawataki kitibiwa katika vituo vya afya na badala yake wanaenda katika Hospitali ya Wilaya ambayo ina utaratibu maalum wa kupokea wagonjwa na wakati mwingine wagonjwa wanakuwa ni wengi kuliko uwezo wa Hospitali hali inayopelekea malalamiko hayo.
Salama,akizungumza changamoto ya baadhi ya wananchi kuchelewa kuungiwa umeme alieleza kuwa shirika la umeme Zanzibar (ZECO) limekuwa likifanya juhudi za kuimarisha huduma zao na kwa sasa wanaendelea na mchakato wa kutatua changamoto hizo za ucheleweshwaji wa kuungiwa umeme ili kumaliza malalamiko ya ukosefu wa huduma hizo.
“Tumepokea maelekezo ya Sekretarieti tutayafanyia kazi kwa wakati,,,pia wananchi wenyewe nao wanatakiwa kubadilika tunavyo vituo vya afya mbalimbali katika wilaya ya Micheweni lakini hawaendi naamini Hospitali ya Wilaya ndio yenye uwezo wa kutoa huduma bora wakati huduma hizo hizo zinapatikana hata katika vituo vya afya.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya itikadi,uenezi na mafunzo CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis amewataka wananchi wa Pemba kupuuza kauli za viongozi wa ACT-wazalendo kupotosha kuwa Serikali haijafanya mambo ya maendeleo kisiwani humo na badala yake wapime maendeleo yaliyotekelezwa na Serikali chini ya Uongozi wa Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Mwinyi na wafanye maamuzi ya kuipigia kura CCM na kuhakikisha inashi nda uchaguzi mkuu wa 2025.
Amesema viongozi wa ACT-Wazalendo wamekuwa wakipotosha na kuendelea siasa za ubaguzi dhidi ya Serikali ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kujali maisha ya wananchi ambao ustawi wa maisha yao unategemea amani,utulivu na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
Amesema viongozi wa ACT-Wazalendo wameishiwa na hoja badala yake wamekuwa wakifanya siasa za ulaghai na fitna zisisokuwa na nafasi katika ulimwengu wa siasa za kisayansi zinazozingatia utafti,tathimini na hoja zinazotafsiriwa kwa maendeleo ya vitendo sio ahadi hewa.
“Wanachama na wananchi wote wa kisiwa cha Pemba hakuna cha kumdai Rais Dk.Mwinyi,ameendelea kuifungua Pemba kiuchumi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayogusa maisha ya watu wa rika zote bila ya ubaguzi.
Tunasikia maneno eti Serikali haijafanya kitu ebu watwambie hizo barabara,shule za ghorofa,bandari za kisasa,matengenezo ya uwanja wa ndege,miundombinu ya maji,uwekezaji katika utalii,boti za kisasa za uvuvi,kupanda kwa bei ya mwani na karafuu na huduma bora za afya na mengine mengi je yamefanywa na Serikali ipi wao watwambie wamefanya nini mpaka hivi Sasa”,alihiji Mbeto.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya mambo ya siasa na uhusiano wa kimataifa Khadija Salum Ali,amewasihi viongozi hao kuhakikisha CCM inashinda pia wajitokeze kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama hicho kwani kila mwanachama ana haki ya kugombea nafasi yoyote anayotaka.
Akizungumza Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya organazesheni CCM Zanzibar Ibrahim Omar Kilupi,amewaonya baadhi ya wanachama na viongozi mbalimbali walioanza kutoa kauli za vitisho kwa wenzao wanapotaka kugombea na kwamba hakuna mwenye hati miliki ya kuwa kiongozi wa kudumu ndani ya CCM kila mtu anqpata nafasi kwa wakati wake.
Kilupi,amesema tayari CCM ishatangaza ratiba ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu kupitia Wilaya na mikoa ya CCM hivyo wanachama wote wanaopiga kura ya maoni wahakikishe wanachagua viongozi wachapakazi,waadilifu na wenye uzalendo wa kusimamia na kutetea maslahi ya wengi na sio maslahi binafsi.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Micheweni Ali Masoud Kombo,amesema kila mwanachama ana wajibu wa kuhakikisha Chama hicho kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu ujao.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Wajumbe wa Kamati za siasa ngazi za Matawi,Wadi,Majimbo ya CCM Wilaya ya Micheweni katika mwendelezo wa ziara ya ya kuimarisha uhai wa Chama na Jumuiya zake katika ziara yake ya Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC,CCM Taifa Zanzibar huko Micheweni Kisiwani Pemba leo tarehe 28/04/2025.