


Arusha .Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameonyesha kuridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Arumeru, hususan mradi wa kuboresha miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Arumeru na ujenzi wa jengo la utawala la Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, (TICD).
Arusha DC imepokea zaidi ya shilingi bilioni 49.6, na Arumeru imepokea zaidi ya shilingi bilioni 51 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Hili ni jambo kubwa, wananchi wana kila sababu ya kumshukuru Rais kwa jitihada hizi,” amesema Dkt. Biteko.
Ametaja mafanikio yaliyopatikana kupitia uwekezaji huo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme kwa vijiji vingi, ujenzi wa shule, maabara, vituo vya afya, hospitali, miradi ya barabara, pamoja na miradi ya kilimo.
Aidha, amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi chache Afrika ambazo zimefanikiwa kuzalisha umeme kwa asilimia 100.
Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Biteko alieleza kuwa Serikali bado inafanya kazi ya kutatua changamoto zilizopo katika sekta ya maji, barabara na miundombinu mingine.
“Serikali ni sikivu. Tutahakikisha barabara zinazohitajika zinajengwa, daraja na huduma za maji zinapatikana. Tutaendelea kutekeleza miradi yenye tija kwa wananchi,” ameongeza.
Tusijaribu kuichezea amani. Ni msingi wa maendeleo yote. Rais Samia ameapa kuilinda kwa gharama yoyote, na sisi wote tuna jukumu hilo,” amesema Dkt. Biteko.
Katika ziara hiyo, Dkt. Biteko aliweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru.
Mradi huo, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.664, unatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na unatarajiwa kukamilika ifikapo Mei 17, 2025.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Taasisi hiyo ya TICD , Dkt. Bakari George, hadi sasa ujenzi huo umeshagharimu shilingi bilioni 2.7.
Jengo hilo litakuwa na ghorofa tatu na sakafu nne, likiwa na jumla ya ofisi 44 pamoja na kumbi tano zitakazoweza kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja.
Dkt. Biteko yupo katika ziara ya siku tano mkoani Arusha, ambapo tayari ametembelea wilaya za Monduli, Longido na Arumeru, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.