Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wasomi nchini kutokuwa na Upande katika uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili kupata nafasi ya kuieleza jamii ukweli bila kuwa na Unazi.
Dkt. Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Aprili 25,2025 jijini Dodoma wakati akihitimisha maadhimisho ya Kilele cha Siku ya sheria 2025 ya shule kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) iliyoongozwa na Mada isemayo “nafasi ya Kliniki za Sheria za Vyuo Vikuu katika kuhakikisha Uchaguzi Huru,Haki na Uwazi Tanzania”.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi kila mmoja katika jamii anayo nafasi yake ya kufanya uchaguzi wa mwaka huu kuwa huru, haki na wazi lakini uwe wa amani, ila vyuo vikuu vina nafasi zaidi, kwasababu wasomi wa vyuo vikuu mna fursa ya kuangalia mambo katika jicho tofauti, sio jicho la kinazi, sio jicho la kishabiki ila jicho la kitaaluma na kuieleza jamii kweli kwenye mambo kadhaa yanayoendelea kwenye jamii,”amesema.
Aidha Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa suala la uchaguzi ni suala linalohusu haki za binadamu hivyo hakuna anayelazimishwa kugombea wala kupiga kura, vivyo hivyo hakuna mtua anapaswa kuzuiliwa kugombea.
“Unaposema No Reform No election unataka kuwanyima watu haki zao za binadamu kama kugombea na kuchagua, ukisoma ibara ya 5 na 2 ya katiba zinaongelea vizuri suala hilo na hakuna sehemu wameandika No Reform No election,” ameongeza.
Amesema uchaguzi ni zoezi linaloongeza Imani kwa wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi, hivyo waendelee kuwaelimishe wadau wote wa uchaguzi kuheshimu sheria za uchaguzi zilizopo, zilizopitishwa na Bunge na sio zile wanazozitaka wao.
Naye Naibu makamu mkuu wa chuo cha UDOM- Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Prof. Razack Lokina amesema kuwa maadhimisho hayo ni ya 4 kufanyika huku lengo likiwa ni kuitangaza shule hiyo ya Sheria.
“Miaka mitatu iliyopita Chuo Kikuu kilikubali maombi ya kutoka shule kuu ya sheria ya kuanzisha kliniki ya sheria, kwa ufupi kliniki ya sheria ni mpango maalum wa ufundishaji wa sheria kwa vitendo na ni sahihi kufanani kliniki ya sheria na maabara zinazotumiwa upande wa sayansi kama utabibu au kemia,”amesema.
Kwa upande wake Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Amina Ally amesema mbali na kuhitaji uchaguzi wa Haki na Uwazi ila jambo la msingi ni kulinda amani ya nchi.
“Amani ni kitu kikubwa sana nchini kabla na baada ya uchaguzi, sisi wananchi tuna wajibu wa kila mmoja wetu ni vyema kuhakikisha kwamba tunakwenda kushiriki kwenye uchaguzi, pia ni jukumu letu kuanza kuelimishana kuanzia kwenye familia,”amesema.