Mwenyekiti wa Halmashauri ya Magu,Mpandalume Simon,lo akifungua kikao cha Baraza la Madiwani, robo ya tatu ya mwaka 2024/25.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mpandalume Simon, akiendesha kikao cha robo ya tatu mwaka 2024/25 cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo,leo.
Watumishi na wadau wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, wakiwa katika kikao cha madiwani leo.
Madiwani wa Halmashauri ya Ilaya ya Magu, wwakiwa katika kikao vha robo tatu ya maka 2024/25, leo wamsikiliwa mwenyekiti (hayupo pichani). Picha na Baltazar Mashaka.
……………

NA BALTAZAR MASHAKA, MAGU

Halmashauri ya Wilaya ya Magu imepata mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hadi kufikia mwaka 2024/25 mapato ya ndani yameongezeka kutoka sh. bilioni 2.4 mwaka 2021 hadi kufikia  bilioni 5.2 kwa mwaka.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo,Mpandaule Simon,amesema leo wakati wa kikao cha robo ya tatu cha Baraza la Madiwani, ambapo alieleza kuwa ongezeko hilo la mapato limechochea utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kimkakati, hususan katika sekta ya elimu na afya.

Amesema walipoingia madarakani mwaka 2020/21, kulikuwa na udhaifu mkubwa uliosababisha halmashauri kukusanya sh.bilioni 2.4 za mapato ya ndani,lakini kutokana na mikakati na usimamizi mzuri wa makusanyo katika vyanzo, mwaka uliofuata walikusanya sh.bilioni 3.6 na baadaye bilioni 3.8.

Simon amesema udhibiti wa ukusanyaji wa mapato na matumizi ya fedha za miradi uliiwezesha Halmashauri ya Magu, kukusanya sh.bilioni 5.2 ambapo kwa miaka minne mfululizo imepata hati safi baada ya taarifa ya ukaguzi ya CAG.

 “Haikuwa kazi rahisi eneo la mapato ya ndani,tuliweka mkakati wa makusanyo tukiwahusisha watendaji wa wa kata, leo tunakusanya bilioni 5.2 ambapo asilimia 40 ya mapato yetu hayo yametumika kujenga shule 24 za sekondari na shule 11 za msingi katika maeneo mbalimbali ya wilaya,” amesema na kuongeza.

“Ni jambo la kujivunia  na ni hatua kubwa ya  kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu bora na katika mazingira mazuri,.amoja na kupigwa vita na  fitina za kisiasa,madiwani tumefanya kazi kubwa ya kuwatumikia wananchi, binafsi ninayo furaha kubwa  sijawaangusha wana Magu.”.

Simon amesema katika  sekta ya afya, halmashauri hiyo imefanikiwa kuboresha Kituo cha Afya cha Nyanguge kwa sh. milioni 100, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya jirani, kwamba kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya  imefanyika kwa weledi kwa kodi zao pia, kurudisha fadhila kwa kura zao.

Amesema kwa miaka mitano wameimarisha usimamizi wa mapato,wameibua vyanzo vipya ikiwemo stendi ya Kona ya Kayenze,stendi ya zamani inaingiza milioni 31 badala ya milioni 14 huku madini ujenzi yakiingizia halmashauri sh.milioni 54 hadi 60 kutoka sh. milioni 22 kwa mwaka.

Mwenyekiti huyo wa Halmashauri na Diwani wa Nyigogo (CCM) ameipongeza  Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiunga mkono halmashauri hiyo kwa vitendo .

Naye Diwani wa Sukuma (CCM), Faustine Makingi amesema serikali kuu imejenga shule ya wasichana ya sekondari ya Magu Girls yenye hadhi ya kisasa kwa sh. bilioni 3, sambamba na kuleta zaidi ya sh.milioni 850 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za msingi.

“Tumepiga hatua kubwa katika sekta ya elimu tumepandisha ufaulu na hakuna sifuri.Afya huduma zimesogezwa karibu na wananchi, tunamshukuru Rais wetu kwa moyo wake wa kuwekeza katika maendeleo ya wananchi, hasa kwenye elimu na afya. Haya ni mafanikio makubwa ambayo kila mwananchi wa Magu anapaswa kujivunia,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Diwani wa Viti Maalum, Stella Anthony, mafanikio hayo ukiemo ujenzi wwa zahanati saba  ni kielelezo cha usimamizi bora wa rasilimali, uwazi katika matumizi ya fedha za umma, na ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa halmashauri na wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Magu (DED),Mohamed Ramadhan,amesema fedha zote za mapato ya ndani zitaingizwa benki na kutumika kwa matumizi sahihi pia, mapato fungwa hadi kufikia juzi Ijumaa imebaki asilimia saba kufikia lengo  ambapo halmashauri hiyo imekuwa ya kwanza kitaifa katika matumizi ya mfumo wa GOTOMIS katika utoaji wa huduma za afya.