Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliianzisha Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius K. Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kwa lengo la kuenzi maono ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere, Muasisi na Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa vitendo.
Hayo yamesemwa mkoani Mara, Aprili 24, 2025, na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alipotembelea chuo hicho.
Prof. Nombo ameeleza kuwa hadi kufikia Mei 2023, Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetoa TSh. 2,661,998,500.00 kwa ajili ya ukarabati wa Kampasi ya Oswald Mang’ombe, ambapo kwa sasa imedahili wanafunzi 78 wanaoendelea na masomo, huku baada ya ukarabati kampasi hiyo ikitarajiwa kuweza kuchukua wanafunzi 300.
Aidha, amesema kuwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation – HEET) inatekeleza ujenzi wa kampasi 16 mpya za vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini ikiwemo MJNUAT.
Kupitia Mradi MJNUAT imetengewa kiasi cha dola za Kimarekani 44,500,000 (sawa na Tsh. 102,500,000,000.00) kwa ajili ya Ujenzi wa kampasi mbili—Butiama na MJNUAT Kampasi ya Tabora katika Kijiji cha Itonjanda ili kuongeza fursa za elimu ya juu.
kupitia Mradi huo pia Chuo kitasomesha wahadhiri, kupitia na kuandaa mitaala inayoendana na uhitaji wa soko.
Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa kwa kuzingatia kuwa kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya nguvu kazi inategemea kilimo, MJNUAT itachangia kwa kiwango kikubwa katika sekta ya kilimo, utafiti na ajira.
Chuo hicho kinatarajiwa kuwa kiungo muhimu katika kuendeleza tafiti za kisayansi zinazohusiana na kilimo, teknolojia za kilimo, na maendeleo ya kilimo cha kisasa na chenye ustahimilivu.