Baadhi ya Wakulima wa kahawa katika kijiji cha Kingerikiti Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma wakiondoa majani yasiyofaa kwenye shamba la kahawa ili kupata kahawa bora.
Baadhi ya Wakulima wa kahawa katika kijiji cha Kingerikiti Halmashauri ya Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma wakiondoa majani yasiyofaa kwenye shamba la kahawa ili kupata kahawa bora.
Afisa Ushirika wa Wilaya ya Nyasa Mkoani Ruvuma Menas Komba kulia,akizungumza na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kingerikiti,wakati wa ziara yake ya kutembelea vyama vya Ushirika katika vijiji mbalimbali Wilayani humo.
Na Mwandishi Maalum,Nyasa
Wakulima wa zao la kahawa katika kijiji cha Kingerikiti Wilaya Nyasa Mkoani Ruvuma,wameishukuru Serikali kwa kusimamia bei ya zao hilo kwenye soko la Dunia kutoka Sh.3,000 mwaka 2021/2022 hadi kufikia Sh.8,500 kwa kilo moja,bei iliyoleta mafanikio makubwa katika maisha yao.
Vitus Mapunda alisema,miaka ya nyumba hawakupata mafanikio makubwa kwenye zao la kahawa kwani gharama ya uzalishaji zilikuwa kubwa wakati bei ya kahawa ilikuwa ndogo,hivyo kuwa na maisha magumu licha ya jitihada kubwa wanazofanya mashambani.
Alisema,katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita bei ya kahawa imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka na hali hiyo imetokana na usimamizi mzuri unaofanywa na Serikali kuanzia kwenye maandalizi ya msimu wa kilimo,ukuaji wa kahawa,wakati wa mavuno hadi wanapopeleka sokoni.
Alisema,kabla ya mpango wa kutoa mbolea za ruzuku unaotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita mavuno katika shamba lake yalikuwa kati ya tani nne hadi tano tu kwa ekari moja,lakini sasa mavuno yameongezeka na kufikia tani kumi.
Alisema,licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye tasnia ya kahawa,lakini changamoto kubwa ni maafisa ugani kutowafikia wakulima kwa haraka ili kuwapa elimu ya kilimo cha kisasa ambacho kitakuwa na mchango mkubwa kiuchumi kwa mkulima na Serikali kwa ujumla.
Ameiomba Serikali,kupeleka maafisa ugani kila kijiji ili waweze kuwafikia wakulima wengi mashambani badala ya kuishia ngazi ya kata na makao makuu ya Halmashauri na kuwaacha wakulima wakiendelea kulima kwa mazoea jambo linalorudisha nyuma uzalishaji wa mazao.
Mkulima mwingine wa kijiji hicho Gabinus Mapunda alisema,alianza kujishughulisha na kilimo cha kahawa kwa muda mrefu, lakini hakupata mavuno mengi kama ilivyo katika kipindi hiki cha Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Alisema,mafanikio aliyoyapata yamechangiwa na mifumo rahisi ya upatikanaji wa pembejeo hususani mbolea na dawa za kuuwa wadudu ambazo awali ziliuzwa kwa bei kubwa ambayo wakulima walishindwa kununua.
Ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya kilimo kwa kuimarisha Ushirika kwani sasa wakulima wanafaidi matunda yake kuanzia kwenye uzalishaji hadi wakati wa mauzo ya kahawa na mazao mengine yaliyoingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.
“elimu ya kilimo bora na elimu ya Ushirika tunayopata kutoka kwa wataalam wetu inatusaidia sana kuelewa namna ya kuvitumia vyama vyetu vya Msingi vya Ushirika(Amcos)kuuza mazao tunayolima kwa bei nzuri”alisema Kapinga.
Alisema,miaka ya nyuma walikuwa wananunua mbolea kwa bei kubwa kwa kutoka kwa wafanyabiashara binafsi,lakini sasa wanapata pembejeo kwenye Amcos zao kwa bei ndogo ikilinganishwa na bei wanazouziwa na wafanyabiashara wa mitaani.
Kapinga,ameishauri Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya Nyasa kuhakikisha maafisa ugani wanakuwa karibu na wakulima ili kuwapa elimu hatua itakayosaidia kuongezeka kwa uzalishaji mazao mashambani.
Mkulima wingine wa kijiji hicho Sarafina Mbele,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuwezesha mbolea za ruzuku ambazo zimechangia sana kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la kahawa na kusimamia vizuri Ushirika ambao umesaidia wakulima kunufaika na mfumo wa kuuza mazao kupitia stakabadhi ghalani.
Katibu wa Chama cha Msingi cha Ushirika wa kilimo na masoko Kingerikiti Fabian Ndunguru,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa ushirikiano mzuri nan chi mbalimbali Duniani kwani kupitia ushirikiano huo Amcos yao imepata ufadhili kutoka Nchi ya Marekani kiasi cha Sh.milioni 588,037,302.00.
Ndunguru alisema,kati ya fedha hizo Sh.milioni 79,824,622.00 zitatumika kujenga maabara ya kahawa,mgahawa,sehemu ya kukaanga kahawa pamoja na ghala la kuhifadhi kahawa.
Kwa upande wake Afisa Ushirika wa Wilaya ya Mbinga Menas Ndomba,amewataka wakulima kuzingatia uzalishaji wa kahawa wenye tija,kuzingatia ubora na kutouza kahawa ikiwa bado shambani kwa bei ndogo.