Na. Leah Mabalwe, NALA
Shule ya Sekondari Nala imefanikiwa kupandisha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi kutokana na utekelezaji wa dhamira ya serikali ya awamu ya sita wa kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya chakula na lishe shuleni.
Kauli hiyo ilitolewa na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nala, Mwl. Joseph Chambo alipokuwa mwenyeji wa waandishi wa habari waliotembelea shule yake kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo na utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni hapo katika kipindi cha miaka minne ya serikali.
“Katika utekelezaji wa Muongozo wa kitaifa wa ulaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi wa elimumsingi umetunufaisha sana. Hapo awali kulikuwa na mahudhurio hafifu sana shuleni kwetu. Pia hata tukiwa darasani wanafunzi walikuwa na uelewa wa chini na hata ufaulu ulikuwa sio mzuri sana. Kufuatia utelekezaji wa mwongozo huu shule yetu sasa imekuwa ni ya mfano. Watoto wanahamasika kuja shule na hata ufaulu umepanda kwa kiasi kikubwa kulinganisha na hapo awali. Sisi kama walimu tumetekeleza muongozo huo kwa kiasi kikubwa sana’’ alisema Mwl. Chambo.
Vilevile, aliongeza kuwa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni hapo ulisaidia kuepusha vishawishi kwa wanafunzi hasa wanafunzi wa kike. “Huduma ya chakula na lishe imesaidia kuchochea wanafunzi kuja shuleni na kusoma kwa amani na utulivu huku wakifuatilia vipindi kwa umakini, jambo lililopelekea kupanda kwa kiwango cha ufaulu” alisema Mwl. Chambo.
Nae, Mwanafunzi Vanessa Fidelis aliishukuru serikali kwa utaratibu wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe shuleni hapo.
“Naishukuru sana serikali kwa kuleta huduma hii shuleni kwasababu imesaidia kuhamasisha wananfunzi kupunguza utoro na imesaidia kusoma kwa muda mrefu hasa vipindi vya jioni. Utaratibu huu umesaidia kukuza taaluma yetu na kupandisha kiwango cha ufaulu” alisema Fidelis.