Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Aprili 17, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari – MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Gideon Gregory, Dodoma.
Waziri wa nchi,Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe.George Simbachawene amesema miongoni mwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka Minne ya serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 205 kimeokolewa na kurejeshwa serikalini.
Waziri Simbachawene ameyasema hayo leo Aprili 17,2025 Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa habari juu ya mafanikio ya wizara hiyo katika kipindi cha miaka hiyo ya serikali ya awamu ya sita.
“Fedha hiyo imepatikana kutokana na kuimarishwa kwa TAKUKURU iliyopelekea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi hadi kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa nchini ambapo sehemu ya fedha hiyo imetumika kutekeleza miradi mingine ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa Serikali imeimarisha uwezo wa kiutendaji wa taasisi hiyo kwa kuiwezesha rasilimali watu, rasilimali fedha, vitendea kazi pamoja na mafunzo ya weledi kwa watumishi, kati ya mwaka 2022 na 2024, Serikali iliipatia TAKUKURU vibali vya ajira 1,190 na kugharamia mafunzo ya weledi na ya kimuundo kwa watumishi wake.
Mbali na hilo amesema Tanzania imeendelea kufanya vizuri kwa kupata alama 41 na kushika nafasi ya 82 kati ya nchi 180, ikiwa imepanda kwa nafasi Tano ikilinganishwa na alama 40 kwa mwaka 2023 na kushika nafasi 8, ambapo imeendelea kushika nafasi ya pili katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yameiwezesha Tanzania kutambuliwa kitamataifa katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA Serikalini ambapo mwaka 2022, Benki ya Dunia ilifanya utafiti katika nchi 198 Duniani kuhusu Ukomavu wa Matumizi wa Teknolojia Duniani katika Utoaji wa Huduma za Serikali na Ushirikishwaji wa Wananchi (GovTech Maturity Index).
Sambamba na hayo amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 35.9 kimetolewa kama mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi waliyokuwa wamebuni wanufaika wa mradi wa TASAF kutoka kaya za walengwa zilizokidhi vigezo.
“TASAF imetoa mafunzo ya stadi za msingi za shughuli za kiuchumi za ruzuku ya uzalishaji kwa kaya za walengwa zilizokidhi vigezo, hadi kufikia mwezi Desemba, 2024, walengwa 94,520 kwenye Mamlaka na maeneo ya utekelezaji 69 walikuwa wamepewa ruzuku ya uzalishaji ya kiasi cha shilingi bilioni 35.9 kama mtaji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi waliyokuwa wamebuni,”amesema.