Na WMJJWM- Sirari Mara
Serikali inapeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi bila upendeleo wowote ule kwa kuzingatia uhitaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi katika maeneo yao.
Hayo yamebanishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu wakati akizungumza na wananchi wa Kata za Tarime Vijijini Aprili 16, 2025 ikiwa ni muendelezo wa Kampeni ya Mageuzi ya Kifikra na Mtazamo wa kuwafanya wananchi kuwa kitovu cha maendeleo yao.
Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan haina upendeleo wowote kwa sababu inazingatia Mpango wa Maendeleo wa Serikali na vipaumbele vyake vilivyopo katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Nawasisitiza wananchi wenzangu tuwe wazalendo kwa kushiriki katika miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yetu, miradi hii hailetwi kwa upendeleo bali ni mahitaji ya msingi kwetu tuithamini” ameeleza Mdemu.
Aidha akiwa katika Kata ya Nyamongo Naibu Katibu Mkuu Mdemu ameshiriki ujenzi wa shimo la choo katika shule ya Sekondari Ingwe na kutoa mchango wa mifuko ishirini (20) ya saruji ikiwa ni moja ya mifano ya kuhamasisha wananchi kuwa na mtazamo wa kujiletea maendeleo.
Naye Mwananchi wa Kata ya Gorong’a Tatu Ramadhani ametoa shukurani kwa Serikali kwa kuwafikia na kuwapa elimu itakayowabadilisha kifkra na mitazamo yenye tija katika kujipatia maendeleo.
“Tunashukuru sana kwa elimu hii mliyotuletea leo, tunaomba iwe endelevu, leo tumeyajua makubwa yanayofanywa na Serikali kwa ajili yetu, tumetambua fursa nyingi zimewekwa kwa ajili yetu na tunahaahidi kuzitumia” amesema Tatu.
Katika Kampeni hiyo Naibu Katibu Mkuu Mdemu ameambatana na wataalam mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii wakiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Patrick Golwike ambao wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi pamoja na kuwashirikisha fursa za maendeleo ndani ya maeneo yao.